WATUMISHI WAPYA NA WALIOHAMIA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI WAPIGWA MSASA

Imewekwa: 28 Nov, 2025
WATUMISHI WAPYA NA WALIOHAMIA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI WAPIGWA MSASA

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendesha mafunzo elekezi kwa watumishi wapya na waliohamia katika Ofisi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Utumishi wa Umma. Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 28 Novemba, 2025 Jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Divisheni ya Utawala na Rasilimali watu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Faith Minani amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha Watumishi hao kuyafahamu majukumu, utendaji kazi, utamaduni pamoja na miongozo ya Utumishi wa Umma.

“Katika mafunzo haya Watumishi watapata fursa ya kupitishwa kwenye Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, majukumu yanayotekelezwa na Divisheni na Vitengo vyetu na watajifunza masuala mbalimbali kuhusu Utumishi wa Umma.” Amesema Bi Faith.

Akiwasilisha mada kwa Watumshi hao, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Leila Muhaji amewaeleza Watumishi hao kuhusu majukumu yanayotekelezwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini pamoja na umuhimu wa mawasiliano katika taasisi, na  pia aliwasisitizia kupata habari sahihi za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia kurasa rasmi za Ofisi za mitandao ya kijamii na tovuti. 

“Niwaombe muwe Mabalozi wazuri wa kuitangaza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na pia  kufuatilia kurasa zetu za mitandao ya kijamii ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kufahamu na  kupata habari sahihi ” Amesema Bi. Leila .

Aidha, Wakili wa Serikali Mwandamizi Bw. John Kinuno akimuwakilisha Mkurugenzi wa Mikataba na Makubaliano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akizungumza katika mafunzo hayo ameelezea juu ya Muundo wa Divisheni ya Mikataba, maana na malengo ya kufanya Upekuzi wa Mikataba, hatua muhimu za kufuatwa na Sheria mbalimbali zinazowaongoza katika Upekuzi wa Mikataba.

“Ni muhimu kwa Wakili wa Serikali kuzingatia Sheria na taratibu zote wakati anapofanya kazi ya Upekuzi wa Mikataba, Wakili anatakiwa awe na uelewa mpana wa Mkataba husika anaoufanyia Upekuzi, hii itamuwezesha kutoa opinion sahihi kuhusiana na Mkataba husika.” Amesema Bw. Kinuno.

Naye, Wakili wa Serikali Mwandamizi Bw. Ladislaus Komanya kwa niaba ya Mkurugenzi wa Divisheni ya Uratibu na Huduma za Ushauri wa Kisheria amewaelezea Watumishi hao juu ya namna Divisheni hiyo inavyotekeleza majukumu yake pamoja sehemu (Section) zilizoko katika Divisheni hiyo, ambapo ameeleza kuwa Divisheni hiyo ina jukumu kubwa la Utoaji wa Ushauri wa Kisheria kwa Wizara, Divisheni zinazojitegemea,  Wakala, Taasisi  za Serikali na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Katika hatua nyingine, Afisa Tehama Bw. Herman Chibegeja alitoa wasilisho kuhusiana na masuala mbalimbali yanayohusu mifumo ya TEHAMA iliyoko katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali sambamba na majukumu yanayotekelezwa na Kitengo cha TEHAMA.

Kwa upande wake, Afisa Tawala Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala, Bora Bi. Stella Teri amewasisitiza watumishi hao kuzingatia Sheria, Kanuni, na Taratibu za Utumishi wa Umma, ikiwemo maadili, nidhamu, na namna bora ya kutoa huduma kwa umma.

“Nitoe wito kwenu kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma, mkafanye kazi kwa nidhamu na kufuata maadili, na mzingatie suala la kutoa huduma bora kwa wananchi.” Amesema Bi. Teri .

Watumishi wapya na waliohamia katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliopewa mafunzo elekezi juu ya majukumu ya Ofisi na miongozo ya Utumishi wa Umma wameapa Kiapo cha Ahadi na Uadilifu kitakachowasaidia kufanya kazi kwa weledi, uaminifu, na uwajibikaji.