Ni yepi Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali?
Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yanaelezwa katika Ibara ya 59(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Sura ya 268, pamoja na Tangazo la Serikali Namba 48 la mwaka 2018. Pamoja na majukumu mengine, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inawajibika kutoa ushauri kwa Wizara, Idara za Serikali na Taasisi nyingine za Serikali, na Mashirika ya Umma kuhusu mchakato wa kutunga sheria na ushauri wa kisheria katika masuala ya jumla na katika uandaaji wa miswada kwa ajili ya kupitishwa na Bunge ili kuwa sheria.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatumia mikakati gani kuhakikisha jamii inapata elimu ya masuala ya kisheria na pia inafahamu Sheria zilizorekebishwa.?
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Kamati za Ushauri za Mikoa na Wilaya pamoja na Kliniki za Sheria, inaendelea kutoa elimu ya sheria bure kwa wananchi. Aidha, Ofisi inaendelea kutoa elimu hiyo kupitia vyombo vya habari. Pia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko mbioni kugawa Sheria zilizotafsiriwa kwa kugha ya Kiswahili bure kwa wananchi wakati wa Kliniki za Sheria.
Mawakili wa Serikali hawapatikani katika ngazi za vijiji na mitaa hivyo viongozi wa serikali za mitaa ndio watatuzi wakubwa wa migogoro, je ni kwa kiwango gani mmewapa uelewa wa Kisheria viongozi hawa?
Ofisi imeanzisha Kamati za Ushauri wa Kisheria katika Mikoa na Wilaya ili pamoja na mambo mengine, Kamati hizi hutoa elimu kwa viongozi hao ili wawahudumie wananchi mahala walipo na kumaliza migogoro katika ngazi tajwa.
Artificial Intelligence (AI) inakuja kwa kasi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga vipi kwa upande wa Sheria ili kukabiliana na mabadiliko haya ya teknolojia?
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga vyema kwa kuwapatia mafunzo ya Akili Mnemba/Unde Mawakili wa Serikali ili wawe na uelewa huo wa kutosha.
Je ni mikakati gani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya muda mrefu ambayo mnatamani iweze kuwafikia wananchi.?
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanzisha Kamati za Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya. Kamati hizo kwa kushirikiana na Ofisi yetu, zinaendesha Kliniki za Sheria ili kusogeza huduma za Kisheria karibu na Wananchi. Ofisi pia ipo mbioni kuanzisha Kituo cha Huduma kwa Wateja (contact center) ili kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa njia ya simu na kidijitali. Lengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kuwezesha huduma hizi muhimu bila malipo ziwafikie wananchi wengi zaidi katika maeneo ya wilayani, vitongoji na vijiji.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ina mpango gani katika kutumia mifumo ya kidigitali kufikisha kazi zake kwa wananchi?
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeboresha Mfumo wake wa OAG-MIS ili kuruhusu Mikataba na Ushauri wa kisheria kuwasilishwa na taasisi za serikali kwa njia ya kidijitali.
Ni maeneo gani ya kipaumbele ambayo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeyapa kipaumbele kuyafanyia kazi kwa miaka mitano ijayo?
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na maeneo mengine imejipanga kutekeleza malengo ya miaka mitano kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa kiasi gani Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) wanasaidia jamii hususan kwa wale ambao hawana uwezo?
TPBA inashirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Katiba na Sheria katika kuhakikisha wanawafikia wananchi wanaohitaji msaada wa huduma za kisheria.
Je Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) na TLS wanakutana wapi kutoa huduma za Kisheria?
Wanachama wa TPBA ni wanachama pia wa TLS. Pia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inashirikiana na Vyama hivi vya kitaaluma katika masuala mbalimbali zikiwemo Kliniki za Ushauri wa Kisheria ambazo hutoa huduma za ushauri wa kisheria kwa wananchi.
Kuna changamoto gani katika utungaji wa Sheria, kwanini Sheria ndogo ndogo ni nyingi?
Sheria Ndogo ni nyingi kwa kuwa kazi yake kubwa ni kufafanua kwa kina zaidi vifungu vya Sheria Kuu.
Kwanini Mikataba ina USIRI, kuna changamoto gani kupelekea Mikataba iwe ya SIRI?
Mikataba inakuwa na usiri kwa sababu ina vifungu ambavyo vinaweka masharti kwa pande zote mbili kutunza siri na iwapo upande mmoja utatoa siri hiyo, unaweza kushtakiwa kwa kukiuka vifungu hivyo.