“UCHAGUZI MKUU WA 2025 NI HALALI” – MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

Imewekwa: 28 Oct, 2025
“UCHAGUZI MKUU WA 2025 NI HALALI” – MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amesema kuwa, Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani 2025 unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba, 2025 ni halali kwakuwa umefuata misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria za Uchaguzi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo katika Mkutano na Vyombo vya Habari uliofanyika Ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma, tarehe 28 Oktoba, 2025.

Akizungumza katika mkutano huo Mhe. Johari amesema kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2025 ni kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa, ni haki ya kila Mtanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

“Ibara ya 5(1) ya Katiba yetu inatoa haki kwa kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane kupiga kura katika uchaguzi unaofanywa Tanzania na Wananchi.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewakumbusha wananchi kuwa kutokana na masharti yaliyowekwa na wananchi katika katiba, Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, unafanyika kila baada ya miaka mitano kama ilivyoanishwa katika Ibara za 42(2) na 65(1) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na Kifungu  cha 56(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024.

“Naomba mfikishe ujumbe kwa wananchi wote kuwa, miaka mitano imeshamalizika kwa mujibu wa Katiba na sasa uchaguzi wa kesho upo kwa mujibu wa Katiba hiyo na kwamba wagombea wote wa nafasi ya Urais, Ubunge na Udiwani nchi nzima wamepatikana kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo uchaguzi huu ni HALALI.” Amesema Mhe. Johari.

Vilevile, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametumia Mkutano huo kutoa onyo kwa wote wanaopanga kuvuruga au kushawishi wananchi kutokushiriki uchaguzi ni kosa kisheria kwa mujibu wa Kifungu cha 129 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.

“Wale wote ambao wamepanga au wanapanga kuandamana, kuleta fujo na kuzuia wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura waache nia hiyo ovu, kwani watakuwa wanatenda kosa la jinai na Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa mujibu wa sheria zilizopo”. Ameeleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali 

Sambamba na hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa wito kwa Wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliotimiza umri wa miaka 18 watumie haki yao ya Kikatiba kwa kujitokeza katika vituo vya kupigia kura ili waweze kuchagua viongozi wao ambao wataongoza nchi kwa niaba yao.

“Mimi nikiwa ndiye Mshauri Mkuu wa Serikali katika  masuala ya Sheria  hapa nchini, daima nitasimamia Katiba na Sheria za Nchi ili kuhakikisha nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya kisheria.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unatarajiwa kufanyika nchi nzima tarehe 29 Oktoba, 2025 kwa Watanzania kuchagua viongozi wao.