TUMIENI SANDUKU LA MAONI KUTOA MADUKUDUKU YENU-AG FELESHI

Na Mwandishi Maalum
Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amekuwa na kikao kazi na Watumishi wa Kada zote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali .
Katika Kikao Kazi hicho na ambacho ni cha Kwanza cha aina yake kimefanyika siku ya Alhamisi katika ukumbi wa mikutano ulipo katika Jengo la Mkapa Jijini Dodoma.
Mhe MMS ametumia kikao kazi hicho kufahamiana na watumishi, kuwapongeza kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yao ya kila siku na vilevile kukumbushana masuala mbalimbali.
Amewaeleza watumishi hao kuwa, kutokana na mazingira ya utekelezaji wa majukumu , imekuwa si rahisi sana kukutana wote kwa pamoja, kusalimiana na kuzungumza, “wengine wapo Ipagala wengine wapo Mtumba, kwa hiyo kunachangamoto kidogo ya ufinyu wa mahali pa kukutana ninaomba jengo jipya likamilike mapema”akaeleza MMS Feleshi.
Akaongeza kwa kusema zimebakia siku chache kabla hajatimiza mwaka mmoja tangu alipoteuliwa na Mhe. Rais kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na kama wanafamilia ameona kunahaja na umuhimu wa kuwa na kikao kazi hicho na watumishi wote.
“Kwanza niwapongeze kwa kazi nzuri , pamoja na changamoto mbalimbali mmekuwa mkitekeleza majukumu yenu vizuri ingawa katika utekelezaji wa majukumu hayo kuna maumivu mnapitia lakini kazi zinaendelea niwapongeze katika hili “ akasitiza Mhe. MMS ana kupigiwa makofi na watumishi.
Baadhi ya masuala ambayo MMS amesisitiza katika kikao kazi hicho ni umuhimu kuendelea kuweka mazingira ya kila mtumishi katika Divisheni na kitengo ajue kinachoendelea katika Divisheni au Kitengo kingine. Kwa kile alichosena Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiyo nyumbani kwa watumishi wenyewe, kwa serikali na wadau wengine.
Na akawataka watumishi kuishi kama familia moja, kujithamini , kujitambua, na kuvumiliana.
Akawakumbusha Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo kujijengea utamaduni wa kuwafahamu watumishi waliochini yao na kwa kufanya hivyo wataweza kutambua uwezo wa kila mmoja wao lakini pia kufahamu changamoto mbalimbali wanazopitia iwe za kikazi au za kifamilia.
Mhe. Feleshi amewahimiza pia watumisishi kulitumia sanduku la maoni kutoa madukuduku yao au kwenda kwa watu wanaowamini. Na kusisitiza kwa mara nyingine hapendi majungu.
“Mtu asijione hana furaha, hii Ofisi ni ya kila mtu hivyo kila mmoja wetu ajione ana umiliki wa Ofisi na tufanye kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma” Amesisitiza Mhe. AG.
“ Ukishapewa Ofisi fanya kazi haki zako za kiutumishi zipo tu, kila mmoja wetu ajiamini katika eneo lake la kazi kwa kuchapa kazi hata kama upandishwaji wa daraja lako unachelewa wewe chapa kazi kwani haki zako za kiutumishi zipo palepale” amesema
Kuhusu watumishi wanaokaimu Divisheni au Vitengo amewataka kujiamini katika nafasi hizo badala ya kukaa nusu nusu.
Vile vile amewakumbusha na kuwahimizi watumishi wote matumizi ya E- Office katika utekelezaji wa majukumu na kwamba dunia hivi sasa inaachana na kukimbizana na majalada.
Pamoja na matumizi ya TEHAMA amesisitiza kwa kila Afisa anayekwenda safari za kikazi kuandika taarifa ya safari hiyo mara anaporejea Ofisi.
Sambamba na hilo amerejea tena umuhimu wa watumishi kujiendeleza kwa faida yao lakini pia amesisitiza maendeleo ya kitaaluma yaendane na maendeleo katika ngazi ya familia na katika hili amesisitiza haja na muhimu kukamilishwa kwa sera ya mafunzo na kuimarishwa kwa Sheria Saccos pamoja na kuongeza idadi ya wanachama.
Ametilia umuhimu wa watumishi wote kujifunza namna bora ya kuandika Wasifu wao ( CV) kwa kile alichosema wengi hawajui kuandika wasifu zao na wakiacha mambo ya msingi yanayoiongezea uzito wasifu huo. Pia wawe na utamaduni wa kuboresha wasifu zao kila mara.
Kuhusu Mkutano Mkuu wa Mawakili utakaofanyika mwishoni mwa Mwezi wa Septemba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewataka watumishi wote kushiriki kikamilifu katika mkutano huo, mkutano ambao mgeni Rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akatumia pia fursa hiyo kuipongeza Kamati ya maandalizi ya Mkutano huo.
Mhe. Feleshi ametaka kufanyika mkutano wa wafanyakazi wote angalau mara mbili kwa mwaka.
Katika hatua nyingine amemuagiza Mkurugenzi wa Mipango kuanza mapema maandali ya bajeti ya mwaka wa fesha 2023/24.
Awali akimkaribisha Mwanasheria Mkuu kuongeza na watumishi, Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Francis Kayichile alisema watumishi waliohudhuria kikao hicho walikuwa zaidi ya 80 kati ya watumishi wote. Na kwamba wengine hawakuhudhuria kutoka kuwa nje ya Ofisi kwa shughuli za kikazi.
mwisho