OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAIMARISHA UWEZO WA MAWAKILI KATIKA MIKATABA YA KIMATAIFA

Imewekwa: 25 Nov, 2025
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAIMARISHA UWEZO WA MAWAKILI KATIKA MIKATABA YA KIMATAIFA

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kuwaongezea Mawakili wa Serikali ujuzi katika maeneo muhimu ya kitaaluma, ikiwemo mikataba ya kimataifa ya biashara, sheria za usuluhishi wa kimataifa, pamoja na masuala ya mafuta na gesi. Hatua inayolenga kuboresha utendaji wao katika kusimamia na kutekeleza miradi ya kimkakati yenye manufaa kwa Taifa.

Akifungua mafunzo hayo leo, Novemba 24, 2025 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Uratibu na Huduma za Ushauri, Bi. Neema Ringo, amesema mafunzo hayo yameandaliwa mahususi kuongeza uwezo wa Mawakili wa Serikali katika kuingia na kusimamia mikataba ya kimataifa inayohusiana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Bi. Ringo ameeleza kuwa mafunzo hayo yataimarisha uwezo wa Mawakili wa Serikali katika kuzuia na kutatua migogoro, hususani katika sekta ya gesi na mafuta, sambamba na kuwajengea umahiri zaidi katika kufanya majadiliano ya kitaalamu.

“Mawakili wa Serikali ni washauri wakuu wa Serikali, hivyo ni muhimu wawe na uelewa mpana wa sheria za kimataifa zinazoongoza mikataba mikubwa  ya kimkakati ambayo Serikali huiingia wakati wa kutekeleza miradi ya kimkakati,” amesema.

Amewahimiza washiriki  kushiriki kikamilifu na kubadilishana uzoefu, huku akibainisha kuwa mafunzo hayo ni uwekezaji muhimu katika kuboresha utendaji wao na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mkufunzi wa mafunzo hayo ni Kampuni ya Clyde & Co, ambayo imeingia makubaliano ya ushirikiano na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa lengo la kukuza uwezo wa wataalamu wake na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kisheria.