TUME YA MADINI YAWAPIGA MSASA  MAWAKILI WA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI.

Imewekwa: 16 Sep, 2025
TUME YA MADINI YAWAPIGA MSASA  MAWAKILI WA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI.

Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamekutana na Tume ya Madini na kufanya mafunzo  yanayolenga wajibu wa kisheria na Usimamizi wa Sekta ya Madini Tanzania ambayo yanafanyika  tarehe 15 mpaka 18 Septemba 2025, Jijini Dodoma. 

Kwa Niaba ya Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno, Bi. Neema Ringo Mkurugenzi wa Uratibu na Huduma za Ushauri, amefungua rasmi mafunzo  kwa kuonesha umuhimu wa mafunzo hayo kwa Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Mafunzo haya ni muhimu kwa sababu ya kuwawezesha Mawakili wa Serikali kuelewa wajibu wa Kisheria wa Tume ya Madini chini ya Sheria ya Madini, Sura ya 123 [R.E. 2023], kwa ajili ya kusimamia na kudhibiti rasilimali za madini nchini kwa lengo la kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.” Amesema Bi. Neema.
 
Bi. Neema  ameelezea umuhimu wa Sekta ya Madini katika ukuaji wa uchumi wa Taifa,  ni  muhimu kushirikiana katika usimamizi wa Sheria na Sera katika  taasisi ya Tume ya Madini na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Ninafahamu kuwa Sekta ya madini ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia ukuaji wa uchumi wa Taifa, mapato ya Serikali na ajira kwa Watanzania. Hivyo, mafanikio ya sekta hii yanategemea kwa kiwango kikubwa usimamizi madhubuti wa Sheria na Sera, pamoja na mshikamano wa kitaasisi kati ya Tume ya Madini na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”amesema Bi. Neema.

Awali Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo akimkaribisha Mgeni Rasmi, alielezea umuhimu wa mafunzo haya kwa mawakili wa serikali kutoka kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwani yatawasaidia na kuongeza uelewa katika utoaji wa ushauri wa kisheria.

“Baada ya Mafunzo haya, tunatarajia mawakilii wetu wa Serikali watapata uelewa mkubwa wa shughuli za Madini ambapo itawasaidia katika shughuli zao za kila siku kwa maana utoaji wa Ushauri Kisheria wa mambo mbali mbali ikiwemo masuala yanayohusu Madini.” Amesema Mhandisi Lwamo.

Mafunzo ya Mawakili wa Serikali kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yameandaliwa na Tume ya Madini na yatafanyika kwa siku 4, tarehe 15 hadi 18 Septemba, 2025 Jijini Dodoma.