“SISI OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI TUNAAMINI NYINYI WAHARIRI NI ASKARI WA KALAMU” - NAIBU MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ina amini kuwa Wahariri wa Vyombo vya Habari ni Askari wa Kalamu kwakuwa wanauwezo wa kuelimisha, kulinda na kusimamia masuala mbalimbali yanayogusa Jamii ikiwemo misingi ya Sheria na Utawala Bora.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini tarehe 11 Septemba, 2025 Jijini Dodoma.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa Vyombo vya Habari katika kujenga Utawala Bora na Uwazi ambapo amesema kuwa Vyombo vya Habari ni daraja muhimu la kuunganisha Serikali na wananchi, na ndio maana ni muhimu sana kwa wahariri kuwa na uelewa wa kutosha wa masuala ya kisheria ili waweze kuripoti kwa usahihi na bila upotoshaji.
“Sisi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tunaamini nyinyi Wahariri wa Vyombo vya Habari ni Askari wa Kalamu kama tulivyo sisi Mawakili wa Serikali, kwakua mna jukumu muhimu la kulinda na kusimamia misingi ya Utawala Bora kwa kutoa taarifa sahihi kwa wananchi.” Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika hatua nyingine, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kupitia kikao hicho Wahariri watapata uelewa wa kutosha wa majukumu yanayotekelezwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia mada zitakazolenga kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kisheria hususan katika maeneo ya Ushauri wa Kisheria, Uandishi wa Sheria pamoja na Majadiliano na Upekuzi wa Mikataba.
“Ni matarajio yetu kuwa, mtakuwa huru kutoa maoni yenu yatakayorahisisha uelimishaji katika kuripoti masuala ya kisheria na hatimaye kusaidia kuondoa baadhi ya upotoshaji unaoweza kujitokeza katika kuripoti taarifa za kisheria”. Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Aidha, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea kufanya maboresho mbalimbali ya Sheria ili ziweze kuakisi malengo ya utekelezaji wa Dira 2050 ambapo ameeleza kuwa maboresho hayo yanafanyika kwa lengo la kuendana na mabadiliko ya Kijamii na Kiuchumi kufikia Dira 2050.
“Kwa upande wetu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tunahakikisha maelekezo ya Mhe. Rais yanatekelezwa kwa ufanisi na weledi mkubwa kwa kuhakikisha tunaoanisha Sheria tulizonazo na kule tunakotaka kwenda ili ziakisi malengo ya Dira 2050.“ Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Awali, akizungumza kwa Niaba ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Rodney Thadeus amewataka Wahariri wa Vyombo vya Habari kukitumia kikao kujifunza masuala mbalimbali ya kisheri yatakayoelezwa kwenye kikao hicho ili waweze kutoa taarifa zilizo sahihi na zenye masilahi kwa taifa.
“Ndugu zangu Wahariri wa Habari tuendelee kusimamia misingi na weledi ya Uandishi wa Habari ili tuweze kuripoti taarifa kwa usahihi na weledi mkubwa“. Amesema Bw. Rodney
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inafanya kikao na Wahariri wa Vyombo vya Habari kwa siku mbili ambapo kikao hicho kimeanza tarehe 11 na kitaendelea hadi tarehe 12 Septemba 2025.