OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YASHIRIKI MKUTANO WA 63 WA AALCO

Imewekwa: 15 Sep, 2025
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YASHIRIKI MKUTANO WA 63 WA AALCO

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeiwakilisha Tanzania kushiriki Mkutano wa 63 wa Shirika la Mashauriano ya Kisheria kwa Nchi za Asia na Afrika (AALCO) uliofanyika tarehe 8 hadi 12 Septemba, 2025 Jijini Kampala Uganda.

Nchi wanachama wa Shirika hilo zimekutana kwa lengo la  kujadili masuala mbalimbali ya kisheria hususani  Kinga kwa Wakuu wa nchi dhidi ya jinai, Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Uhalifu wa Mitandao, na ripoti ya utekelezaji wa majukumu ya vituo vya usuluhishi vya AALCO.

Akizungumza kuhusiana na Mkutano huo Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi. Florentina Sumawe amesema kuwaTanzania imeshiriki mkutano huo kwa kuwasilisha mada juu ya hatua zilizochukuliwa katika Utekelezaji na Uzingatiaji wa Mikataba ya Kikanda na Kimataifa inayohusu Biashara na Uwekezaji, Sheria ya Bahari, Mazingira na Maendeleo Endelevu, Urejeshaji wa Mali zinazotokana na Uhalifu, na Utatuzi wa Migogoro kwa njia mbadala.

Katua hatua nyingine, Bi. Sumawe amesema kuwa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika mkutano huo yalikuwa kuhakikisha usahihi wa taarifa za kisheria zilizopo kwenye nyaraka zilizowasilishwa na kutoa ushauri wa kisheria pale ulipohitajika.

Aidha, Bi. Sumawe ameeleza katika mkutano huoTanzania ilitoa pendekezo kwa Shirika la AALCO kuhusu uandaaji wa mfumo wa makubaliano ya kisheria (Model Investment Treaty). Mfumo huu utatumika kama mwongozo wakati wa majadiliano na uandaaji wa mikataba ya uwili (bilateral) na kimataifa (multilateral) ya Uwekezaji.