OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAIMARISHA USHIRIKIANO NA PURA

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekusudia kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa uweledi na ubora, ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali juu ya namna ya kuboresha utendaji kazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), ili kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wananchi na wadau waliowekeza katika sekta ya mafuta na gesi.
Akizungumza leo, Oktoba 15, 2025, wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali, yaliyofanyika katika Ofisi ya PURA, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni, amesema kuwa mafunzo hayo ni fursa ya kubadilishana uzoefu kati ya PURA na Mawakili wa Serikali kuhusu utekelezaji wa majukumu ya udhibiti katika Mkondo wa Juu wa Petroli.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Silinde Gumada amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia Mawakili wa Serikali kuifahamu kwa undani PURA na namna inavyotekeleza majukumu yake, jambo ambalo litaboresha utendaji wao katika kushughulikia masuala ya kisheria yanayohusu PURA.
Wakili Gumada ameongeza kuwa uelewa wa shughuli za PURA utasaidia pia kuepusha migogoro kati ya Serikali na wawekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, pamoja na kuongeza ufanisi na weledi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
"Itawasaidia Mawakili wa Serikali kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi kwa kuielewa vizuri PURA, kuboresha mahusiano ya kikazi, na kuishauri Serikali juu ya njia bora za kuimarisha utendaji wa PURA ili iweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi na wadau," amesema Wakili Gumada.
Katika mafunzo hayo, Mawakili wa Serikali watapata fursa ya kujifunza kuhusu historia ya PURA tangu kuanzishwa kwake, sheria zinazosimamia Mkondo wa Juu wa Petroli, usimamizi wa mikataba, ukaguzi wa mahesabu ya mikataba ya Uzalishaji wa Pamoja (PSA), pamoja na ushiriki wa Tanzania katika sekta ya mafuta na gesi asilia katika Mkondo wa Juu wa Petroli.