NAIBU MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA JENGO LA  OFISI  MWANZA

Imewekwa: 08 Jul, 2025
NAIBU MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA JENGO LA  OFISI  MWANZA

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno, tarehe 04 Julai, 2025 amefanya ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali unaoendelea katika eneo la Buswelu Jijini Mwanza.

Ziara hiyo imelenga kukagua na kuona hatua iliyofikiwa katika mradi huo ambao umefikia asilimia 70 ambapo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tayari imelipa Asilimia 87 ya gharama za ujenzi huo  unaotarajiwa kukamilika  mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2025.

Aidha, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amepokea taarifa ya kazi zinazoendelea kufanyika kwa sasa iliyowasilishwa na Eng. Sirudi A. Sanga kutoka Suma JKT na Mshauri Mwelekezi  Arch. Salum H. Kihelo kutoka TBA ikiwa ni pamoja na 'skimming, uwekaji wa tiles maeneo ya vyoo  na jikoni 'blandering'  pamoja usiimikaji wa miundombinu ya umeme.

Vilevile, Mhe. Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amekagua  mpango kazi wa mkandarasi na hatua iliyofikiwa kwa kila kazi na kumuelekeza mkandarasi huyo kuongeza kasi ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati.

Katika hatua nyingine Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameridhishwa na maendeleo na hatua iliyofikiwa katika  mradi huo wa ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa tatu.

Katika ziara hiyo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameambatana na Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Bw. Elias Kisamo, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi Bi.Proscovia Ichwekeleza,  Bi.Beatrice Nzobonaliba kwa niaba ya Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Wakili wa Serikali Bw. Nyamhanga Nyamhanga pamoja na  Wakili wa Serikali  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mwanza Bw. Kabyemela S. Lushagara