MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA WANASHERIA KUONGEZA UMAKINI KATIKA KUTOA USHAURI WA SHERIA ZA MAZINGIRA

Imewekwa: 04 Sep, 2025
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA WANASHERIA KUONGEZA UMAKINI KATIKA KUTOA USHAURI WA SHERIA ZA MAZINGIRA

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amewataka Wanasheria kuwa walinzi na kuongeza umakini katika kutoa ushauri wa sheria zinazohusu mazingira kwa maslahi ya taifa.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo tarehe 3 Septemba, 2025 wakati akifungua mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kuhusu sekta ya mazingira yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira  (NEMC) Jijini Dodoma.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema wanasheria hao wanatakiwa kuwa walinzi na kuongeza umakini katika kutoa ushauri wa sheria za mazingira kwa maslahi ya nchi.

“Natambua zipo changamoto wakati wa utekelezaji ,mfano uelewa mdogo wa masuala ya mazingira hivyo tunawajibu wa kuzibadili changamoto hizi na kuzifanya fursa kwa kuimarisha nafasi ya NEMC katika kusimamia sheria katika sekta ya mazingira.”Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alimshukuru Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kwa kuweka utaratibu  huu wa mafunzo kwa mawakili wa serikali.

“Nimshukuru Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuweka utaratibu huu mzuri wa mafunzo haya ya mawakili wa serikali kwa namna hii kiuweledi kwa kuwagawa mawakili wa serikali katika makundi yani claster mbali mbali ili wapate ubobezi katika hizo clasters likiwemo hili la mazingira” amesema Mh. Johari.

Mhe. Johari amesema mafunzo hayo yatawasaidia  Mawakili hao wa Serikali kuelewa vizuri sheria  na taratibu zinazohusu usimamizi wa mazingira na kufahamu majukumu ya NEMC  na sheria zinazohusu ada na tuzo za kisheria.

Vilevile Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameongeza kuwa mafunzo hayo yataongeza uelewa kwa Mawakili wa Serikali hivyo kuwasaidia wakati watakapokuwa wanatoa Ushauri wa Kisheria na Upekuzi wa Mikataba inayohusu hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.

Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya tathmini ya mifumo ya kitaasisi ili kuboresha utendaji, kwa sasa lipo andiko linalochakatwa lenye lengo la kuibadili NEMC kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Sambamba na hilo Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa NEMC inatakiwa kuandaa kanuni na viwango vya ada vinavyozingatia uhalisia wa gharama za huduma pamoja na kusimamia na kudhibiti uzalishaji wa taka na uchafuzi wa mazingira na kutoza ada za udhibiti.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisisitiza jinsi ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilivo tayari kushirikiana na taasisi zingine katika kuhakikisha inafikia malengo yake katika Dira  ya maendeleo ya taifa 2050.

“Ofisi yangu ipo tayari kushirikiana na NEMC katika taratibu zote za kisheria na katika kufanikisha lengo hili sambamba na zoezi zima la kuoanisha sheria zetu kuakisi malengo ya dira ya taifa 2050” anasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Awali, Mkurungenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira Tanzania (NEMC) Dkt. Immaculate Semesi amesema kuwa wameandaa mafunzo hayo kwa lengo la kujengeana uelewa wa kisheria za usimamizi wa mazingira nchini.

Pia, Dkt. Semesi anasisitiza ushirikiano huu wa NEMC na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali utawezesha kukamilisha malengo yote ya Dira ya Taifa 2050 kwani mazingira ni nguzo ya tatu katika dira 2050.


“Pia kama mnavotambua tuna dira yetu ya taifa 2050 na moja ya nguzo kuu kabisa katika dira hii nguzo ya tatu ni suala zima la mazingira, kwa kushirikiana na tutambue  mazingira ni uhai kwa sababu yanatuwezesha kufanya shughuli zote za maendeleo”. Anasema Dkt Semesi.