WAOMBA OMMS KUANDAA MAFUNZO ENDELEVU KUHUSU MIRADI YA PPP

Dodoma-Naibu Mwanasheria Mkuu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Shaaban Ramadhan Abdalla ameelezea kuridhishwa kwake na mafunzo waliyopewa ya kuwajengea uelewa kuhusu miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ( PPP).
Amesema mafunzo hayo yamekuwa na umuhimu hasa kwa upande wa Zanzibar ambako serikali ya awamu ya nane imeamua kufungua milango ya uwekezaji.
“mafunzo haya yamekuwa ya muhimu sana kwetu sote na hasa sisi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar ambako Serikali ya Awamu ya Nane imefungua milango kwa wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, na ndiyo maana tumekuja washiriki 20 kwenye mafunzo hayo ambao wanatoka Divisheni ya Mikataba”.
Naibu Mwanasheria Mkuu Shaaban Ramadhan Abdalla ameyasema hayo wakati wa uhitimishaji wa mafunzo ya siku nne ya kuwajengea uwezo na uelewa kuhusu miradi ya PPP mafunzo ambayo yameratibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na kwa ufadhili wa Taasisi ya Kimataifa ya African Legal Support Facility (ALSF).
Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Mikutano ulipo katika Hoteli ya Dodoma jijini Dodoma. Jumla ya washiriki 60 kutoka Taasisi mbalimbali wakiwamo Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Pamoja na kuelezea kuridhishwa na mafunzo hayo ambayo watoa mafunzo walikuwa ni wataalamu kutoka Taasisi ya Pinsent Massons Bw. John Woolley na Bw. Jonathan Hart,Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar itaendelea kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo Bi Nzeyimana Dyegula kutoka Shirika la Reli Tanzania ( TRC) pamoja na kupongeza kuwapo kwa mafunzo hayo ameomba na kushauri Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kuratibu mafunzo ya aina hiyo kwa kushirikiana na wadau wake.
Akasema mafunzo ya uandaaji, utekelezaji, usimamia na ufuatiliaji wa miradi ya PPP ni muhimu sana na yanatakiwa kuwa endelevu hasa kutokana na miradi hiyo kuwa na changamoto nyingi.
“Kwa niaba ya washiriki wenzangu kwanza nisema tunaishukurua Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa uratibu wa mafunzo haya kwa kushirikiana na ALSF, mimi binafasi nimekuwa nikishughulikia miradi hii ya PPP kwa Zaidi ya miaka sita sasa, lakini nikiri kwamba bado nakumbana na changamoto nyingi kwa hiyo tunapopatiwa mafunzo kama haya siyo tu tunajifunza mambo mapya lakini pia tunajifunza na namna ya kukabiliana na changamoto” akasema Bi.Dyegula
Aidha amesema kutoka na unyeti wa miradi ya PPP mafunzo yakuwajengea uwezo wataalamu pamoja na Mawakili wa Serikali ni muhimu sana na kwamba yeye binafsi amefurahishwa na mchanganyiko wa wataalamu waliohudhuria mafunzo haya.
“Kwa mara ya kwanza nimehudhuria mafunzo haya kuhusu miradi hii ya PPP pasipokutana na mtu ninaye mfahamu tofauti na huku nyuma semina au mafunzo ya aina hii utakuta watu ni wale wale lakini hapa ni tofauti na hii inatupatia fursa ya kujifunza na kubadilishana uelewa kwa upana zaidi.
Aidha washiriki hao wamesema mafunzo haya yamekuwa mazuri zaidi kwa sababu wakufunzi walikuwa ni wanasheria wenzao na hivyo kuongea lugha wanayoelewana na yalikuwa shirikishi.
Haya ni Mafunzo ya awamu ya pili kuratibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na ALFS ya mafunzo ya awamu ya kwanza yalihusu masuala ya madini, gesi na mafuta.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano
6/7/2023