Wakili wa Serikali Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Benson Makala akipokea cheti cha ushiriki wa mafunzo kuhusu gesi, madini na mafuta

MAFUNZO YAMETUONGEZEA MAARIFA- WAHITIMU
Na Mwandishi Wetu
16 Septemba 2022
DODOMA
Mafunzo ya siku nne ya kuwajengea uwezo maafisa wa serikali katika maeneo ya madini, gesi na mafuta yamehitimishwa leo kwa washiriki wa mafunzo hayo kukabidhiwa vyeti.
Jumla ya maafisa 37 wakiwamo wa kutoka Ofisi ya Rais, wameshirikia mafunzo hayo ambayo baadhi yalitolewa wawezaji wa kimataifa kwa njia ya mtandao na mengine yalitolewa na wawezaji Bw. Akshai Fofaria kutoka Kampuni ya Sheria ya PINSENT MASON LLP kutoka London Uingereza na Bw. Aggrey Ernest Kutoka Kampuni ya Sheria ya A&K Tanzania.
Akihitimisha mafunzo hayo Bi Aida Sylla mmoja wa waratibu wa mafunzo hayo kutoka Taasisi ya Kimataifa ya African Legal Support Facility ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuratibu mafunzo hayo na kuahidi tena kwamba Taasisi ya ALSF itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mafunzo hayo kuhusu masuala ya madini, mafuta na gesi ni awamu ya kwanza kati ya awamu tatu ambazo ALSF imeingia makubaliano na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wamesema mafunzo yalikuwa ni mazuri na kwamba katika siku nne hizo za mafunzo wamejengewa uwezo lakini wao wenyewe wamejengeana uwezo kutokana na kwamba mafunzo hayo yalikuwa shirikishi.
“Kwangu mimi kama mchumi mafunzo yameniongezea uwezo na ufahamu wa mambo mengin yanayohusiana na eneo hili ambalo nisema ni nyeti na muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu”. Akasema Bw. Buji Bampebuye ambaye ni Mkurugenzi wa Mipango Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Naye Bi Upendo Ndosi ambaye pia ni mchumi amesema licha ya kwamba mafunzo hayo yameongeza uelewa katika eneo hilo lakini aina ya ufundishaji, fursa za kuuliza maswali, majadiliano katika makundi ni mambo ambayo amesema yamewasaidia sana.
“Watu tulikuwa huru kuuliza maswali na majadiliano katika makundi pia yamesaidia sana katika kuongeza uwezo wa kuelewa. Lakini pia kupitia mafunzo hayo tumejenga networking ambalo ni jambo nzuri pia”. Akabainisha.