VYAMA VYA USHIRIKA SEHEMU ZA KAZI VISAIDIE KUPUNGUZA CHANGAMOTO ZA WATUMISHI –AG FELESHI

Na Mwandishi Maalum
16/8/2022
DODOMA
Mlezi wa Chama cha Ushirika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali “ SHERIA SACCOS” Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Dk. Eliezer Feleshi amesema kuanzishwa kwa vyama vya ushirika maarufu kama Saccos sehemu za kazi kulilenga katika kuwasaidia watumishi kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwamo ulipaji wa ada za watoto wao.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo wakati alipokuwa akifungua Mkutano wa Wanachama wa Sheria Saccos akiwa ni mlezi wa Chama hicho. Mkutano huo umefanyika leo Jumanne katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Ipagala Jijini Dodoma.
Katika Mkutano huo na ambao pia umehudhuriwa na Maafisa Ushirika kutoka Jiji la Dodoma, pamoja na mambo mengine wanachama watafanya tathmini na kujaidili changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili Saccos hiyo pamoja na kuweka mikakati madhubutu ya kuifufua tena na kuifanya iwe imara kama kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Kwanza, niwapongeze sana kwa kufanya mkutano huu, hii ilikuwa hamu yangu ya muda mrefu mkutane ili pamoja na mambo mengine mjadiliane na kuweka mikakati madhubuti kuhusu Saccos yetu. Nimefarijika sana” akasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mlezi huyo wa Sheria Saccos amebainisha kuwa vyama vya ushirika vilitiliwa mkazo sana na Hayati Mwalimu Julius Nyerere na baadaye Hayati Rais Benjamin Mkapa ambaye naye alihimiza sana kuwa, pamoja na kipato kinachotokana na mshahara, mtumishi awe na shughuli ya kujiingizia kipato kwa kujipatia mitaji kutoka Saccos hizo.
“Hakuna mtu anayependa kuishi maisha ya shida, kila mtu anapenda kuishi kwa furaha. Vyama hivi vya ushirika vitusaidie kuishi kwa furaha kwa kutusaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwamo za kulipa karo za wanafunzi na mambo mengine. Kwa hiyo, kama mlezi ningependa kuona Saccos iliyo imara na inayosaidia kupata suluhu la changamoto za watumishi”. Akasema AG Feleshi.
Mlezi huyo wa Sheria Saccos amebainisha pia kwamba katika kuifanyia mageuzi makubwa Sheria Saccos ni vema wanachama hao kupitia mkutano huo wakajadiliana pia namna ya kuvutia wanachama wapya ikiwani ni pamoja na kuwarejesha waliowahi kuwa wanachama.
Hata hivyo amesisitiza kwamba, ili kuwa na saccos imara na yenye kuwanufaisha wanachama ni muhimu kuwa na viongozi na wanachama waadilifu.
“Nisisitize pia suala ya maadili kwa viongozi na wanachama, ni bora mkabaki wachache waadilifu kuliko kuwa na wanachama wengi wavurugaji. Baadhi ya wanachama wanapokuja kuomba mkopo mikono inakuwa mbele wakishapata mikopo inakuwa shinda”.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia amebaisha kwamba licha ya changamoto ambayo Sheria Saccos imepitia, bado inabaki kuwa Saccos yenye heshima kutokana na viongozi wengi wakiwamo Wanasheria Wakuu wa Serikali waliopita, Wakurugenzi wa Mashtaka waliopita, wanasheria wengi na ambao wengine sasa ni majaji kuwa wanachama wa Saccos hiyo.
Akabinisha pia kuwa, akiwa mlezi wa Sheria Saccos itakuwa aibu sana kusikia kwenye Sheria Saccos kuna ubadhirifu wa fedha na kwa sababu hiyo atasimima sana suala la uadilifu.
Aidha amewataka Maafisa Ushirika kuwa karibu na vyama vya Ushirika ili pamoja na mambo mengine kubaini mapema changamoto na kuzitafutia ufumbuzi mapema.
Awali Afisa Ushirika Yusuf Timotoli akizungumza wakati wa mkutano huo, amesema Sheria Saccos inakabiliwa na changamoto kama ilivyo kwa Saccos nyingine nyingi zilizohamia Dodoma kutoka Dar es Salaam
Hata hivyo amesema Ofisi yao imejitahidi kusaidia katika kuzifufua baadhi ya Saccos ikiwamo ya Utumishi na sasa watahakikisha wanaisimamia kwa karibu Sheria Saccos ili ifikie ubora wake.
Naye Mwenyekiti wa Sheria Saccos Bw. Richard Mbaruku amesema Sheria Saccos ilikuwa na Wanachama 91 lakini waliopo sasa na ambao wapo hai ni 49. Wanachama wa Sheria Saccos ni wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Tume ya Kurekebisha Sheria.