TUMIENI VIZURI UPATIKAJAJI WA FEDHA KUKAMILISHA UJENZI- HAZINA

TUMIENI VIZURI UPATIKAJAJI WA FEDHA KUKAMILISHA UJENZI- HAZINA
Na Mwandishi Wetu
Mtumba- Dodoma
01-06-2022
Wataalamu kutoka Idara ya Tathmini na Ufuatiliaji wa Matumizi ya Fedha, Wizara ya Fedha na Mipango, wamemshauri Mkandarasi ( SUMA JKT) anayejenga jengo jipya la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba, kuhakikisha anaitumia vema fursa ya upatikanaji wa fedha za mradi kutoka serikalini kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi za mradi.
Wametoa ushauri huo siku ya Jumanne, wakati wataalamu hao Bw.Elirehema Mollel na Bw. Lucipine Kahunduka wakiambatana na baadhi ya maafisa wa OMMS walipofika eneo la ujenzi kwa lengo la kupata taarifa za ujenzi wa mradi huo pamoja, kufahamu kama fedha zinatolewa kwa wakati na changamoto mbalimali zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi.
Kabla ya kutembelea eneo la mradi wataalamu hao walikutana na Kamati ya Ujenzi ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo walipatiwa taarifa ya mradi ikiwamo taarifa ya fedha ambazo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imepatiwa kutoka Serikali Kuu, malipo ambayo yamekwisha fanyika kwa mkandarani na mshauri mwelekezi pamoja na changamoto zilizojitokeza katika hatua za awali za maradi.
“ Katika taarifa mliyotupatia inaonyesha mradi upo nyuma kwa takribani wiki 15 kutokana na sababu mbalimbali, ingawa mmeongeza kasi kupunguza pengo hilo, lakini ushauri wetu ni huu, tumieni fursa hii ya mtiririko mzuri wa fedha kutoka serikalini kwa kwa kuongeza kasi ya ujenzi hata ikiwapasa kufanya kazi usiku na mchana fanyeni hivyo” akasema Bw. Elirehema Mollel
Na kuongeza “ kwa kufanya kazi usiku na mchana na kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi ujenzi utakwenda mbali na hata kwa mfano, pakitokea changamoto ya upatikanaji wa fedha basi muwe mmeshapiga hatua kubwa au kufika mbali”.
Pamoja na kumtaka mkandarasi huyo kuongeza kasi, pia wamemshauri Mshauli mwelekezi kutoka Wakala wa Majengo ya Serikali Bw. Peter Muluki ,kuhakikisha hakwamishi kwa namna yoyote ile ujenzi wa jengo hilo ambalo wataalamu wanasema, ni moja kati ya Majengo makubwa ya Serikali yanayoendelea kujengwa katika Mji wa Mtumba.
“ Tumeelezwa pia kwamba wewe (mshauri mwelekezi) pia ulikuwa sababu ya kuchelewa kwa mradi huu kwa kuchelewa kutoa vibali au michoro, tungeomba kwa hapa ujenzi ulipofikia hatutegemei masuala ya utoaji wa vibali au kubadilisha michoro likajitokeza tena kwa sababu, pamoja na kuchelewesha ukamilishaji wa mradi lakini pia kutaongeza gharama.
Na kwa sababu hiyo,Watalalamu hao wameitaka OMMS, Mkandarasi na Mshauri mwelekezi kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara ili kubaini changamoto na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka na hivyo kutokwamisha mradi.
Akijibu na kutoa ufafanuzi wa hoja za wataalamu hao, Meneja wa SUMA JKT kanda ya Kati Meja Samuel Jambo aliwahikishiaka wataalamu hao kwamba, pamoja na kuwa mradi huo umechelewa kwa wiki 15 lakini kasi wanayoendelea nayo sasa ni nzuri na kwamba, wanafanya kazi zaidi ya moja kwenye mradi bila kusubirisha.
Aidha, amesema pamoja na kuongeza muda kwa kazi, lakini pia wanazo malighafi za kutosha kwa maana ya Nondo, Kokoto wanazotoka Tabora na Cementi na zitakidhi mahitaji ya maradi kwa asilimia 40.
Na kuongeza kwamba kwa kasi wanayokwenda nayo sasa na kama hakutatokea mabadiliko yoyote mradi utakamilka kwa wakati.
Kwa upande wake, mshauri mwelekezi Bwana Peter Muluki amesema, hategemei kwa sasa ujenzi ulipofikia kutokea mabadiliko makubwa ambayo yanaweza kupunguza kasi ya utekelelezaji wa maradi huo au kuongeza gharama.
Akaahidi kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu.
Naye Mkurugenzi wa Divisheni ya Mipango Bw. Buji Bampebuye akizungumza kwa niaba ya wajumbe wengine wa OMMS, amesema, Ofisi imekuwa ikitekeleza wajibu wake kwa kuhakikisha kuwa mara inapo pata fedha kutoka Hazina inapeleka kwa mkandarasi kwa wakati.
Vile vile akabainisha Ofisi imekuwa na vikao vya mara kwa mara vya kufanya tathimini ya maendeleo ya mradi na vikao vya kitaalamu.
Jengo jipya la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali linatarajiwa kugharimu Tshs 26.817,046,474.13. Aidha Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi September 2023.
Mwisho