TPBA YAPATA RAIS MPYA

Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) imemtangaza Wakili Bavoo Junusi kuwa Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali akipokea kijiti kutoka kwa Wakili Amedeus Shayo, Rais aliyemaliza muda wake katika uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika tarehe 15 Aprili, 2025.
Akizungumza baada ya kuapishwa rais mteule wa Chama cha Mawakili wa Serikali amewashukuru Wanachama wa chama hicho kwa kumuamini na kumchagua na kuwaahidi kuyafanyia kazi yale yote waliyoyaanzishwa watangulizi wake.
“Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru sana wanachama wote wa chama chetu kwa kuniamini na kunipigia kura kuwa Rais, nawaahidi kuendelea kukijenga chama chetu na kuwa chama imara zaidi.”
Aidha, Bw. Bavoo amewapongeza viongozi wengine walioshinda katika uchaguzi pamoja na wanachama waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo, huku akiwaomba kuungana na kushikamana katika kuendelea kukijenga chama hicho.
“Tulikuwa kwenye mchakato wa uchaguzi ambao umekamilika kwa chama kupata viongozi wapya niwaombe tuungane na kuendelea kukijenga chama chetu.” Amesema Bw. Bavoo
Viongozi wengine waliochaguliwa katika uchaguzi huo kuunda safu mpya ya uongozi katika chama hicho ni pamoja na Bi. Debora Mcharo Makamu wa Rais, Bw. Addo November Mwenyekiti, Bi. Celestina Kunambi Makamu Mwenyekiti na Bw. Rashid Mohamed Said ambaye anaendela kuwa katibu wa chama hicho