TANZANIA YATAKA USHIRIKIANO KUTOKOMEZA UVUVI HARAMU

Na Mwandishi Maalum
Tanzania imezitaka nchi wanachama wa Taasisi ya Mashauriano ya Sheria ya Nchi za Asia na Afrika (AALCO) kushirikiana katika kumaliza tatizo la uvuvi haramu.
Nchi wanachama wa AALCO wanakutana katika mkutano wao wa 61 unaofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Bali Nusa Dua, Mjini Bali, Indonesia. Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Balozi Kennedy Gaston ameongoza Ujumbe wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mkutano huo.
Katika wasilisho hilo, Tanzania imeeleza kuwa tatizo la uvumi haramu linaziathiri sana nchi za Visiwa Vidogo na Nchi za Maziwa Makuu na hivyo ushirikiano wa kulimaliza tatizo hilo ni jambo linalotaka ushirikiano wa dhati wa nchi wanachama wa Taasisi hiyo.
Pamoja na tatizo hilo la uvuvi haramu, Tanzania pia imesisitia haja na umuhimu wa kulinda raslimali za Bahari kwa ustawi na maendeleo ya nchi wanachama wa AALCO na dunia kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Tanzania imeelezea utayari wake wa kushirikiana na Nchi Wanachama katika kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo katika masuala ya sheria za bahari na uchumi wa bluu pamoja na sheria za biashara na uwekezaji kwa maendeleo endelevu ya dunia.
Katika Mkutano huo wa wiki moja, nchi wanachama zinajadili masuala mtambuka ya sheria za kimataifa hususani katika sheria za Bahari na uchumi wa bluu.
Aidha, nchi hizo pia, zinajadiliana jinsi ya kupambana na uvuvi haramu, sheria za biashara na uwekezaji na utatuzi wa migogoro katika vituo vya usuluhishi wa migogoro vya Kimataifa.
Wanachama pia watajadiliana kuhusu na masuala yenye manufaa kwa AALCO ambayo yapo kwenye agenda ya Kamisheni ya Sheria za Kimataifa ya Umoja wa Mataifa (International Law Commission).
Mkutano huo pia utajadiri suala la uvunjifu wa sheria za kimataifa kwenye maeneo ya Palestina; sheria za utwaaji mali zilizoibiwa , mazingira na maendeleo endelevu.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Balozi Gaston katika mkutano huo ameambatana na Mawakili wa Serikali waandamizi Hassan Nkya kutoka Idara ya Uandishi wa Sheria na Felista Lelo kutoka Idara ya Mikataba.
Maafisa hao wawili wamekuwa wakishiriki mikutano ya kitaalamu ya pembezoni (side events).
Mkutano huu pia ulihudhuriwa na ujumbe kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ambao uliongozwa na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Khatibu Kazungu.
AALCO inawanachama 47.Tanzania ilijiunga mwaka 1973
17/10/2023