Tanzania yaombwa kuridhia baadhi ya Itifaki za Mkataba wa Kimataifa kuhusu masuala ya Nyukilia

Na Mwandishi Maalum
Dodoma
Tanzania imeombwa kuridhia baadhi ya itifaki za mabadiliko ya Mkataba wa Kimataifa wa Ulinzi wa Nyezo za Nyukilia (Convention on the Physical Protection of Nuclear Material).
Ombi hilo limetolewa siku ya , jumatano na Bw. Richard Sseggane kutoka Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomu Duniani ( IAEA) wakati ujumbe kutoka IAEA ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania Profesa Lazaro Busagal ulipoitembelea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali jijini Dodoma na kufanya mazungumzo na Mwandishi Mkuu wa Sheria Bw. Onorius Njole.
Bw. Sseggane amebainisha kwa kueleza kwamba, ingawa Tanzania imeridhia Mkataba huo, (The Convention on the Physical Protection of Nuclear Material) lakini bado haijaridhia baadhi ya itifaki za mabadiliko ya mkataba huo, hivyo basi, wanaiomba Tanzania, kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo ni mdau mkubwa katika mchakato wa uridhiaji wa mikataba ya kimataifa kusaidia.
“Tunaiomba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iendelee kushirikiana na Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania na Wizara husika katika kufanikisha kuridhiwa kwa Itifaki zilizobakia”, akasihi Bw. Richard Sseggane kutoka IAEA.
Ujumbe huo pamoja na kuzungumzia kuhusu Mkataba huo pia walizungumzia mkataba mwingine wa kimataifa wa Utokomezaji wa Vitendo vya Ugaidi wa Nyukilia. “the International Convetion for Suppression of Acts of Nuclear Terrorism".
Aidha Ujumbe huo umeishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kuwa mdau muhimu katika masuala ya nguvu za atomu hususani katika eneo la maboresho ya sheria.
Kwa upande wake, Mwandishi Mkuu wa Sheria Bw. Onorius Njole aliyekuwa mwenyeji wa Ujumbe huo kwa niaba ya Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ameuhakikisha Ujumbe huo kwamba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itakuwa tayari kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika katika eneo hilo.
Aidha Mwandishi Mkuu wa Sheria ameushukuru Ujumbe huo kwa kutoa maelezo ya kina kuhusu Mikataba hiyo ya Kimataifa lakini pia kwa kuitembelea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kutambua nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika masuala yote yanayohusu mikataba ya kimataifa.
Bw. Onorius Njole alitumia fursa hiyo kuelezea majukumu mbalimbali ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yakiwamo ya mapitio ya sheria mbalimbali za kitaifa na kimataifa pamoja na na mchakato wa kuzitafsri sheria hizo katika lugha ya Kiswahili.
Mwisho.
Imeandaliwa na Maura Mwingira
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali