“SIFA TUTAKAZOZIPATA HUKO MBELE NI KWA SABABU TUMESIMAMA JUU YA MABEGA YA KAZI ILIYOFANYWA NA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI” – RAIS SAMIA

Imewekwa: 29 Apr, 2025
“SIFA TUTAKAZOZIPATA HUKO MBELE NI KWA SABABU TUMESIMAMA JUU YA MABEGA YA KAZI ILIYOFANYWA NA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI” – RAIS SAMIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kukamilisha zoezi la Urekebu wa Sheria na kuifanya Serikali ya Awamu ya Sita kuingia katika historia ya kuandika Juzuu mpya za Urekebu.

Rais, Dkt. Samia ametoa pongezi hizo wakati akihutubia viongozi na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya utiaji saini tamko la Sheria zilizofanyiwa Urekebu toleo la Mwaka 2023 iliofanyika Ikulu Chamwino, Jijini Dodoma tarehe 23 Aprili, 2025.

“Tunatoa Shukrani zetu kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kulikamilisha hili na kuifanya Serikali ya Awamu ya Sita kuingia kwenye historia ya kuandika juzuu mpya za Urekebu.” Amesema Rais Samia

Aidha, Mhe. Rais amesema kuwa kukamilika kwa zoezi la Urekebu wa sheria ni hatua muhimu katika maendeleo ya Taifa, kwakuwa upatikanaji wa sheria zilizowekwa wazi na zinazoendana na wakati kutasaidia kuwepo kwa amani na shughuli za kiuchumi kufanyika kwa urahisi.

“Sheria ni kioo cha ustaarabu wa taifa, kukamilika kwa toleo hili ni hatua muhimu katika ustawi wa maendeleo ya taifa letu.” Amesema Mhe. Rais

Mhe. Rais amesema kuwa kukamilika kwa juzuu hizo za sheria kutasaidia kufanya utafiti na kupata uhakika wa sheria inavyosema, hivyo kurahisisha maamuzi na kupelekea upatikanaji wa haki kwa wananchi na kwa wakati.

 

“Juzuu hizi zilizorekebishwa ni muhimu sana katika kuongeza uwazi na zitazidi kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao.”  Amesema Mhe. Rais

Katika hatua nyingine Rais Samia ameiagiza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha kuwa inazitafsiri juzuu za sheria kwa lugha ya Kiswahili ili wananchi waweze kuzisoma na kuzielewa, ili kusaidia wananchi kutambua haki zao na kusaidia kupunguza migogoro mbalimbali.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) ametoa pongezi kwa Rais Samia na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufadhili mradi huo mkubwa wa Urekebu wa Sheria mbalimbali nchini, ambapo mradi huo umetumia Rasilimali fedha na watalaamu wa ndani ya nchi.

“Mhe. Rais nakupongeza kwakuwa mradi huu mkubwa wa Urekebu wa sheria uliofanywa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali umetekelezwa kwa kutumia fedha ndani.”  Amesema Mhe. Majaliwa

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari akizungumza katika hafla hiyo amesema kuwa zoezi hilo la Urekebu wa Sheria, ni urithi wa kisheria kwa wadau wa sekta ya sheria, wadau wa haki na wadau wa utawala bora kwakuwa sheria ni msingi wa haki, amani na maendeleo.

Vilevile, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujumla kwa kufadhili zoezi hilo kwa kutoa fedha na kuijengea uwezo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwajengea uwezo wataalamu waliofanikisha zoezi hilo.

“Kwa namna ya pekee naomba kutumia fursa hii kukushukuru wewe binafsi pamoja na Serikali yako kwa kuwezesha mradi huu wa Urekebu. Hii ni mara ya kwanza kwa mradi huu kufanyika kwa fedha za ndani na Wataalamu wa ndani.”  Amesema Mhe. Johari

Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa kutokana na mageuzi na jitihada mbalimbali zilizofanyika katika usimamizi wa sheria na maboresho ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yamechagiza kwa kiasi kikubwa kukamilika kwa zoezi la Urekebu wa Sheria.

” Maboresho ya kuajiri zaidi ya Mawakili wa Serikali 50 na kuanzisha Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria ni hatua muhimu iliyopelekea kukamilisha kwa zoezi hili.”  Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Tamko la sheria zilizofanyiwa urekebu limesainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu litaanza kutumika rasmi tarehe 1 Julai, 2025.