SERIKALI YAWASILISHA MUSWADA WA MAREKBISHO YA SHERIA MBALIMBALI

Imewekwa: 14 Jun, 2023
SERIKALI  YAWASILISHA MUSWADA WA MAREKBISHO YA SHERIA MBALIMBALI

 

 

 SERIKALI  YAWASILISHA MUSWADA WA MAREKBISHO YA SHERIA MBALIMBALI

 

Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Mhe.  Jaji Dkt.  Eliezer Mbuki  Feleshi amewasilisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya  mwaka 2023 ( The Written Laws ( Miscellaneous Amendments) Bill, 2023.

Akiwasilisha  Muswada huyo Mwanasheria Mkuu  wa Serikali amelieza Bunge kuwa Muswada kama ulivyowasilishwa unapendekeza marekebisho katika  Sheria Nane (8)

Akazitaja  sheria hizo kuwa ni  Sheria ya Usajili wa Wabunifu wa majengo na Wakadiriaji Majenzi sura ya  269 (Architects and Quantity Surveyors ( The Registration) Act,Cap.269;  Sheria ya   Huduma za Habari, Sura ya 229 ( The Media Services Act,Cap.229); Sheria ya Bohari ya Dawa, Sura ya 70 ( The Medical Stores Departiment Act, Cap.70) na Sheria ya Mazishi ya Viongozi wa Kitaifa, Sura ya 419 ( The National Leaders Funeral Act., Cap.419).

Sheria nyingine zilizomo  katika  Muswada huo ni Sheria ya  Reli, Sura ya 170 ( The Railways Act, Cap.170); Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania, Sura ya 277( The Tanzania Forestry Research Institute Act, Cap.277).  Sheria ya Mamlaka na majukumu ya Msajili wa Hazina, Sura ya 370 ( The Treasury Registar ( Powers and Functions) Act, Cap 370); na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura ya 148 ( The Value Added Tax Act, Cap 148)

Akielezea kuhusu  sheria ya  mazishi ya Viongozi wa Kitaifa,  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  amesema “ sehemu ya Tano ya Muswada inapendekeza marekebisho kwenye Sheria ya Mazishi ya Viongozi wa Kitaifa, Sura ya 419 ambapo  kifungu cha 6 kinapendekezwa  kufutwa na kuandikwa upya kwa lengo la kuboresha masharti kuhusu mamlaka ya  Rais kutoa tangazo la  kifo cha  kiongozi au kiongozi  mahsusi aliye madarakani”

 Akasema,  marekebishyo hayo pia yanampa mamlaka  kiongozi mahsusi aliye madarakani kutoa tangazo la  kifo cha kiongozi mahsusi mstaafu.

Dkt. Feleshi amelieleza  Bunge zaidi kwamba, marekebisho ya sheria  hiyo  yanakusudia kutoa mamlaka kwa  Rais kutangaza  tarehe ya maziko ya Rais aliyefariki akiwa  madarakani kuwa ni siku ya mapumziko.

Akasema, lengo la mapendekezo haya  ni kuweka bayana na kutofautisha mamlaka zinazopaswa kutoa matangazo ya  vifo vya  viongozi wa kitaifa na viongozi   mahsusi.

Aidha,  Mwanasheria Mkuu  amebainisha  kwamba,  Vifungu vya 9 na 10 vinapendekezwa kurekebishwa ili kutoa mamlaka kwa kiongozi mahsusi aliye madarakani kutoa tangazo  la kifo cha kiongozi mahsusi mstaafu.

“Lengo la marekebisho haya ni kutambua utaratibu unaotumika sasa ambapo  pamoja na kwamba Sheria imemtaja Rais kama mamlaka ya kutoa tangazo la kifo cha kiongozi mahsusi mstaafu, matangazo ya aina hiyo kwa kawaida yamekuwa  yakitolewa na viongozi mahsusi walio madarakani”.

Pamoja na  maelezo ya ufafanuzi sheria hizo  na sheria nyingine zilizowasilishwa katika  Muswada huo. Mwanasheria Mkuu wa Serikali alilieleza  Bunge kwamba,  kwa mujibu wa kanuni ya 99 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Mwaka 2023, anaomba kutoa hoja kwamba  Muswada wa Sheria ya Marekebishyo ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2023 ( the Written Laws ( Miscellaneous Amendments)  Bill, 2023 ) kama  ilivyorekebishwa kwa mujibu wa Jedwali la Marekebisho ujadiliwe na kupitishwa katika  hatua ya  Kusomwa kwa Mara ya Pili na ya tatu na hatimaye marekebisho yanayopendekezwa yawe sehemu ya Sheria za Nchi