OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI, TASAC ZAKUTANA KUBADILISHANA UZOEFU 

Imewekwa: 15 Aug, 2025
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI, TASAC ZAKUTANA KUBADILISHANA UZOEFU 

Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamekutana na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na kufanya kikao kilicholenga kubadilishana uzoefu kati ya Taasisi hizo mbili,   tarehe 14 Agosti, 2025 Jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Wakili wa Serikali Mwandamizi Bw. Ladislaus Komanya amesema kuwa Mawakili wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wameshiriki kikao hicho na kupata mafunzo kutoka TASAC kwa lengo la kufahamu kwa kina majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na Taasisi hiyo. 

"Sisi kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tumekutana na wenzetu kutoka TASAC kwa lengo la kupata mafunzo mahsusi kutoka kwao ili tuweze kuifahamu TASAC kwa undani, na wametupitisha  katika Sheria na majukumu wanayoyatekeleza".

Aidha, Bw. Komanya amesema kuwa kikao hicho pia kinalenga katika kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya Kisheria na Utekelezaji wake.

"Kikao hiki tutakitumia katika kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Kisheria". 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria wa TASAC Bi. Judith Kakongwe amesema kuwa wamekutana na  kufanya kikao na kutoa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwasababu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni Mdau mkubwa wa TASAC katika masuala mbalimbali yanayohusu sheria.

"Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni wadau wakubwa ambao tunashirikiana nao katika kuandaa Kanuni, Kuhakiki Mikataba na Kuridhia Mikataba mbalimbali ya Kimataifa". Amesema Bi. Judith