NBC WAIALIKA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI KUSHIRIKI MBIO ZA MARATHON

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel M. Maneno amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Benki ya Taifa ya Biashara ( NBC) na kukabidhiwa jezi maalum kwa ajili ya mbio za marathon zijulikanazo kama " NBC Dodoma Marathon 2025."
Makabidhiano hayo yamefanyika tarehe 24 Julai, 2025 katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mtumba jijini, Dodoma.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameipongeza Benki ya NBC kwa kuendelea kushirikiana na taasisi za umma katika kuimarisha ustawi wa jamii kupitia matukio ya michezo.
"Nawapongeza sana NBC kwa kutuona na kutupatia vifaa hivi kwa ajili ya kushiriki katika marathon hii na tunawaahidi kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itashiriki kikamilifu, pia mbio hizi ni njia ya kuonyesha mshikamano na mchango wetu katika maendeleo ya jamii." Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya NBC, Bw. Elvis Ndunguru akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa NBC amezungumzia lengo la marathon ya NBC kwa mwaka 2025 ni kuimarisha mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya uzazi, kuboresha afya ya mama na mtoto na kufadhili wauguzi 100 kwa ajili ya watoto wenye changamoto ya usonji, pia ameahidi kuendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali.
“NBC tunaahidi kuendeleza ushirikiano ulipo baina yetu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa kuwa ofisi hii ni mdau wetu mkubwa”. Amesema Bw. Ndunguru
Katika hafla hiyo fupi ya kukabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa NBC aliambatana na Mkurugenzi wa GSM Foundation Bi. Faith Gugu pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Mawasiliano wa NBC Bw. Godwin Semunyu.
NBC Dodoma Marathon 2025 inatarajiwa kufanyika tarehe 27 Julai, 2025 kwa kuwakutanisha washiriki kutoka sekta mbalimbali wakiwemo watumishi wa umma, wafanyabiashara, wanafunzi na wanamichezo huku sehemu ya mapato ya mbio hizo ikielekezwa katika kuboresha masuala ya Afya