NAIBU MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AONGEA NA WATUMISHI WA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

Dodoma
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Balozi Prof. Kennedy G. Gastorn amekutana na kufanya mkutano na watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OMMS). Mkutano huo uliofanyika tarehe 18 Desemba, 2023 ulihudhuriwa na watumishi wote wa OMMS kutoka Makao Makuu ya OMMS Dodoma na Ofisi zote za kanda.
Akifungua mkutano huo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (NMMS) aliwaeleza watumishi kwamba amefurahi kukutana na watumishi wote wa OMMS na kuwahakikishia watumishi kuwa hoja zote zitachukuliwa na kufanyiwa kazi bila kuangalia aliyetoa hoja husika. NMMS alipata fursa ya kupokea taarifa ya utendaji kutoka kwa Wakuu wa Divisheni na Vitengo walioeleza majukumu na changamoto
wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao. Baadhi ya changamoto zilizobainishwa ni pamoja na upungufu wa watumishi, ukosefu wa magari, ukosefu wa maktaba kwa ajili ya rejea na tafiti.
Wakiwasilisha taarifa za utendaji katika maeneo yao, Mawakili wa Serikali Wafawidhi wa Mikoa ambao ndio Mawakili wa Serikali Wafawidhi wa Mikoa wanaomuwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (MMS) katika Mikoa, wamebainisha kuwa wana jukumu la kumwakilisha MMS katika Kamati mbalimbali za Kisheria zikiwemo Kamati za mitihani, Kamati za Mikoa za Maadili za Mahakama, Kamati za Mikoa za Maadili za Mawakili nk. Majukumu mengine yanayotekelezwa na Ofisi hizo ni utoaji wa ushauri wa kisheria kwa Serikali na wananchi pamoja na kutekeleza majukumu mengine ya kiutawala. Hata hivyo, utekelezaji wa majukumu hayo unakumbana na changamoto ya ukosefu wa watumishi na magari.
Wakili Mfawidhi Mkoa wa Mbeya Bi. Catherine Paul kwa upande wake, alishauri kuwa Mamlaka za Mikoa zikumbushwe kushirikisha kikamilifu Ofisi za Mawakili Wafawidhi katika Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa ili kuhakikisha kuwa Kamati hizo zinashauriwa ipasavyo katika masuala ya kisheria kabla ya kuchukua hatua ili kuepuka kuchukua hatua ambazo wakati mwingine zinakinzana na misingi ya Sheria na kusababisha migogoro.
Eneo jingine ambalo lilisisitizwa na Mawakili hao Wafawidhi ni kuhusu Ofisi kulipia viwanja vilivyokwishapatikana katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi. Baadhi ya mikoa ambayo viwanja vimekwishapatikana ni pamoja na Mkoa wa Njombe ambako Ofisi imepata kiwanja chenye ukubwa wa 2623sqm ambacho kinadaiwa shilingi 10,754,300/=; Mkoa wa Songwe 5925sqm kinadaiwa Shilingi milioni 29 na Rukwa 3462 sqm kinadaiwa shilingi milioni 49.
Kwa upande wake, NMMS aliwashukuru watumishi wote kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakimpatia toka ateuliwe kushika nafasi hiyo. NMMS alitumia fursa hiyo pia kuwakumbusha watumishi kuhusu umuhimu wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi. Aidha, pamoja na mambo mengine, NMMS aliwataka watumishi kuendelea kuboresha utendaji wao. Alisisitiza kuwa kuboresha utendaji hakuna ukomo. Mambo mengine yaliyosisitizwa kuzingatiwa ni ubunifu, weledi, utunzaji wa siri, kutoa kazi kwa wakati na uzalendo. NMMS alisisitiza kuimarisha ushirikianao katika kutekeleza majukumu (Team work) miongoni mwa wa wanyakazi na baina ya Divisheni na Divisheni.
Sambamba na kukumbusha mambo mbalimbali ya kuzingatia katika utekelezaji wa majukumu, NMMS aliagiza utekelezaji wa haraka wa mambo yafuatayo: kutafuta namna bora kuhifadhi nyaraka mbalimbali zilizopo Ofisi ya Dar es Salaam, kutambua na kuandaa taarifa kuhusu mashauri mbalimbali ya ndani ya nchi, kuandaa kanzi data ya mikataba inayowasilishwa katika Ofisi, kuangalia uwezekano wa kuwatumia interns ili pamoja na kuwajengea uwezo wasaidie utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hususani Ofisi za mikoa na mwisho kuangalia uwezekano wa kuwa na online library.