NAIBU MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AHIMIZA UJENZI WA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI UKAMILIKE KWA WAKATI

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel M. Maneno, amefanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali linalojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, leo Julai 10, 2025.
Akiwa katika ukaguzi huo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amemtaka Mkandarasi wa mradi kutoka kampuni ya SUMA JKT, Mhandisi Evance Mwingizi, kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa ili jengo hilo lianze kutumika na kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema matarajio ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kuhamia katika jengo hilo mapema mwezi Oktoba 2025, ambapo kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 75.
Kwa upande wake Mhandisi Evance Mwingizi amezitaja kazi zinazoendelea katika mradi huo ni uwekaji wa mifumo mbalimbali kama vile mifumo ya Umeme, TEHAMA, Hewa, pamoja na eneo la nje ikiwemo maegesho ya magari.