Mwanasheria Mkuu wa Serikali azindua Kliniki ya bure ya Sheria kwa kusikiliza kero za Wananchi

*Mwanasheria Mkuu wa Serikali azindua Kliniki ya bure ya Sheria kwa kusikiliza kero za Wananchi*
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe.Jaji Dkt Eliezer Mbuki Feleshi leo tarehe 26 Juni 2024 amezindua rasmi Kliniki ya huduma bure za sheria katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.
Kliniki hiyo imeandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Mawakili wa Serikali ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutaka viongozi kuwa na utaratibu wa kusikiliza malalamiko ya wananchi ikiwa ni pamoja na kuwaongoza katika taratibu za kupata haki.
Akizindua Kliniki hiyo leo Juni 26, 2024 Jijini Dodoma, Dkt. Feleshi amesema Kliniki itasaidia kusogeza msaada wa huduma za kisheria kwa wananchi na kutatua changamoto mbalimbali zinazohusu kisheria.
Katika hatua nyingine, Jaji Feleshi ametoa maagizo kwa Mawakili wa Serikali kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na kutatua kero za wananchi “Natoa rai kwa Mawakili wote wa Serikali hapa nchini kutenga muda na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi kwa kuwatembelea kwenye maeneo yao, Aidha aliwaomba pia wakuu wa mikoa na Wilaya ambao bado hawajakamilisha kuteua wajumbe wawili wa kamati za ushauri wafanye hivyo ili kamati hizo zianze kusikiliza malalamiko ya wananchi kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa, "amesema.
Katika Kliniki hiyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt Eliezer Feleshi alipata wasaa wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi waliotembelea kwenye mabanda mbalimbali ya huduma za sheria yaliyokuwepo viwanjani hapo.
Mhe. Feleshi pia alisisitiza kuendelezwa kwa ushirikiano baina ya Serikali na kamati za ushauri ngazi za Mikoa na Wilaya, na vyama vya Mawakili wa Serikali (TPBA)pamoja na Mawakili wa Tanganyika (TLS) kuendelea kushirikiana na Serikali kusikiliza malalamiko na kuyatatua kwa wakati.
Aidha Mhe Jaji alitoa wito kwa vyombo vya habari kutangaza Kliniki hiyo kwa wananchi wa Dodoma na maeneo jirani ili wapate huduma ya Ushauri wa kisheria bure kuanzia Juni 26 hadi Julai 3,2024 kuanzia saa 2.00 asuhubi hadi saa 10.00 jioni.