MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA WANANCHI  KUJITOKEZA KUJIANDIKISHA DAFTARI LA WAPIGA KURA

Imewekwa: 16 May, 2025
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA WANANCHI  KUJITOKEZA KUJIANDIKISHA DAFTARI LA WAPIGA KURA

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amezungumza hayo mara baada ya kubadilisha taarifa zake katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura  katika kituo cha  Ofisi ya Mtendaji wa kata Kilimani, Jijini Dodoma, tarehe 16 Mei, 2025.

"Nimekuja hapa kwenye kituo cha kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura nimepata huduma nzuri sana, na ndani ya muda mfupi wamenitengenezea kadi nzuri ya kisasa na yakidigital."

Mhe. Johari amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi hilo ili waweze kutimiza haki yao ya kikatiba na  kujiandikisha kwa ajili ya kuchagua viongozi mbalimbali kwa mujibu wa sheria na katiba, pia amesema zoezi hilo la  kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura linachukua muda mfupi mpaka kukamilika kwake.

"Nichukue fursa hii kuwaasa wananchi wajitokeze kwa wingi kushiriki katika zoezi hili, kwani zoezi lenyewe linachukua muda mfupi wanahakiki taarifa zako na unapata kitambulisho chako kwa haraka".

Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kutumia mifumo ya kisasa na kuandaa utaratibu mzuri unaowaruhusu wananchi kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao kwenye daftari la wapiga kura katika muda mfupi.

"Niwapongeze Tume yetu ya Taifa ya Uchaguzi kwa kazi nzuri wanayoifanya kwani utaratibu ni mzuri na huduma hii inatolewa kwa haraka sana".

Zoezi la kujiandikisha na kuhakikisha taarifa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Dodoma limeanza tarehe 16 Mei, 2025 litaendelea hadi tarehe 22 Mei, 2025.