MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AWAFUNDA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

Dodoma
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OMMS) ilifanya Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi tarehe 19 Desemba 2023. Mkutano huu ulifunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Akifungua Mkutano huo, Mhe. Mchengerwa alimshukuru Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi ambae pia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (MMS) kwa kumualika kuwa mgeni rasmi katika Mkutano huu muhimu pamoja na kumpongeza yeye pamoja na watumishi wa Ofisi hiyo, kwa kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo mkubwa. Aidha, alimpongeza Mh. MMS kwa jitihada mbalimbali ambazo amekuwa akichukua katika kukabiliana na mashauri mbalimbali ya ndani na nje ya nchi dhidi ya Serikali. Jitihada hizi zimesaidia kupunguza mzigo wa gharama zinazotokana na madai ya kesi hizo kwa Serikali. Vilevile, Mhe. Mchengerwa aliishukuru OMMS kutokana na ushirikiano ambao amekuwa akiupata katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara yake hususan katika maeneo ya maandalizi ya Sheria Ndogo za Mamlaka za Serikali za Mtaa na uhakiki wa mikataba.
Mhe. Mchengerwa alisisitiza umuhimu wa kufanya maboresho katika OMMS ili kuhakikisha Ofisi hii inakuwa na ubora unaoendana na maboresho yaliyofanyika upande wa Mahakama. Aidha, pamoja na kupongeza kazi kubwa inayofanyika katika uandaaji wa Sheria Ndogo, alisihii OMMS kuendelea kuimarisha mikakati ya kutatua kasoro mbalimbali ambazo zimekuwa zikibainishwa na Bunge katika taarifa za uchambuzi wa Sheria Ndogo.
Vilevile, aliongeza kuwa mikakati ya pamoja baina ya Wizara yake na OMMS itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kama siyo kuondoa kabisa kasoro katika Sheria Ndogo hizo. Alihiimiza OMMS kuendelea kuunga mkono jitahada za Mh. Rais za vita dhidi ya rushwa, ufisadi na kukosa uzalendo zinazoweza kuharibu taswira ya Ofisi. Pia alieleza umuhimu wa kuweka utaratibu wa namna bora ya kushirikiana na TAMISEMI ili kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali waliopo katika halmashauri 307 Nchini. Alieleza kuwa TAMISEMI imekuwa haifanyi vizuri katika baadhi ya kesi zake katika baadhi ya Mahakama, hali inayosababishwa na mambo mengi hususani kukosa uzalendo na kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Akimkaribisha mgeni rasmi kufungua Mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi alimshukuru Waziri kwa utayari wake na kwa kukubali ombi la kuwa mgeni rasmi katika Mkutano huu. Sambamba na hilo, alimpongeza Mhe. Balozi Profesa Kennedy Godfrey Gastorn kwa kuteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Pamoja na kubainisha ajenda za Mkutano huo, Mhe. Jaji Dkt. Feleshi alieleza kwamba ajenda za Mkutano huu zinalenga kupima mafanikio ya utekelezaji wa mpango na bajeti na mizania ya mahesabu ya mwaka 2022/2023.
Akifafanua baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi husika, Mhe. Jaji Dkt. Feleshi alieleza kuwa, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, OMMS ilifanikiwa kutekeleza Mpango Kazi wake kwa kuongeza watumishi wa OMMS, kuongeza vifaa vya TEHAMA ambapo kwa sasa takribani asilimia 95 ya Watumishi wa Ofisi hiyo wamepatiwa kompyuta mpakato, kutoa mafunzo ya ndani na nje nchi kwa watumishi, kuendesha, kusimamia na kushiriki katika majadiliano na mashauri ya madai na jinai mahakamani, kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya utendaji kazi wa OMMS, kuandaa miswada ya Sheria 17, kutafsiri sheria 319, kufanya zoezi la urekebu wa sheria 741 na sheria ndogo 829, kufanya upekuzi wa mikataba 1,777 na Randama za Maelewano 466, kutoa ushauri wa kisheria kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambapo idadi ya ushauri huo ni 1,252. Upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA umewezesha OMMS kuimarisha matumizi ya TEHAMA hususani katika mfumo wa OAG-MIS ambao umerahisisha utendaji kazi wa OMMS.
Mwenyekiti wa Baraza alieleza kuwa, maboresho ya Muundo wa OMMS yaliyofanyika kupitia Tangazo la Serikali Na. 48 la mwaka 2018 yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji hususan katika utoaji wa ushauri wa kisheria, upekuzi wa mikataba, uandishi wa sheria ndogo na uendeshaji na usimamizi wa mashauri kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Alisisitiza pia katika lengo hilo hilo la kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, maboresho yameendelea kufanyika kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Sekta ya Sheria ambayo imeanzisha rasmi Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Hatua hii itasaidia kuimarisha na kuongeza ufanisi katika masuala ya uandishi wa Sheria.
Mhe. Jaji Dkt. Feleshi alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 OMMS ilianza ujenzi wa majengo ya Vituo Jumuishi katika Mikoa ya Mwanza na Arusha pamoja na ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu Dodoma. Hatua hii inalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kisheria zitolewazo na taasisi husika sehemu moja na hivyo kuwapunguzia gharama wadau na wananchi, kuongeza kasi na wigo wa upatikanaji wa huduma hizo kwa wakati na kupunguza gharama za uendeshaji wa Ofisi kwa kuepukana na gharama za kila taasisi kujenga au kupanga pango lake.
Mhe. Jaji Dkt. Feleshi alisema kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado OMMS inakabiliwa na changamoto za upungufu wa bajeti ya kuendesha shughuli za Ofisi, upungufu wa watumishi, ufinyu wa nafasi za Ofisi na uhaba wa magari ambapo Ofisi ina jumla ya magari 16 yakiwemo magari matatu chakavu wakati mahitaji ni magari 45. Kati ya magari hayo, magari 13 yapo katika hali nzuri na yanatumika na magari 3 ni mabovu na yanahitaji matengenezo. Kwa upande wa watumishi, OMMS inahitaji watumishi 462 huku waliopo ni watumishi 177.
Vilevile, Mhe. Jaji Dkt. Feleshi alieleza uwepo wa dosari za kimaandishi na kimaudhui katika kazi zinazotoka nje ya OMMS na hivyo kuwaelekeza Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo kuhakikisha wanapitia na kujiridhisha na kazi zilizofanywa na maafisa ambao wapo chini yao kabla ya kazi hizo hazijatoka nje ya Ofisi, ili kuimarisha ubora wa kazi hizo na kujenga uaminifu. Aidha, alimuagiza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kuhakikisha watumishi wote wamejisajiri katika Mfumo wa PEPMIS.
Mwisho Mhe. Jaji Dkt. Feleshi alieleza kuwa watumishi wote wa OMMS wanapaswa kufahamu kwamba ni wajibu wetu kuheshimiana bila kujali tofauti zetu za kada na wadhifa tulionao na hivyo, hatua za kinidhamu zichukuliwe mara moja kwa watumishi wa OMMS watakaobainika kuharibu taswira ya Ofisi kwa kujihusisha na vitendo vilivyo kinyume na maadili ya utumishi wa umma. Aidha, alizikumbusha Menejimenti za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na mamlaka nyingine Serikalini kuweka vigezo mahsusi kama vile kuendesha mashauri ya aina mbalimbali kwa idadi itakayokubalika, kufanya tafiti katika maeneo yenye matokeo makubwa na kushiriki kikamilifu katika majukumu yanayopimika atakayopangiwa, ambavyo vitatumika kuwaombea vyeo vya msereleko Mawakili wa Serikali watakaovitelekeza kwa ufanisi pamoja na wasimamizi wao.