MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI ATOA ANGALIZO KWA WATUMISHI MATUMIZI YA TEHAMA

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI ATOA ANGALIZO KWA WATUMISHI MATUMIZI YA TEHAMA
Na Mwandishi wetu.
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi ameelezea matumaini yake kwamba juhudi za kuwawezesha watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa na vitenda kazi vya kutosha vya TEHAMA utawawezesha kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ameyaeleza hayo wakati akimkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ( Mb) kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mkutano huo ulifanyika Aprili 18, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mkoani Dodoma.
Katika taarifa yake kwa wajumbe wa Baraza hilo kuhusu namna uongozi wa OMMS ulivyofanya juhudi za upatikanaji wa vitenda kazi. Mwenyekiti Jaji Feleshi alieleza kwamba kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Ofisi , Ofisi imeweza katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 hadi Machi 2023, Ofisi imeweza kupata komputa mpakato na vishikwamba 160, komputa za mezani 23, printa 5 na fotokopi moja.
“Mhe. Mgeni rasmi vitendea kazi hivi vimesaidia sana kupunguza upungufu mkubwa wa vitenda kazi uliokuwapo. Tunaamini vifaa hivi vitaongeza thamani ya kazi zetu” akaeleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Baraza.
Akabainisha kwamba juhudi hizo za upatikanaji wa vitenda kazi ni juhudi endelevu na lengo hasa ni kuhakikisha kwamba angalau kila mtumishi anakuwa na kitendea kazi kitakachomuwezesha kufanya kazi kijiditali.
Akasema “ tumeshatoa maelekezo ya ndani kwamba ifikapo Julai Mosi 2023 Ofisi yetu itakuwa kwenye matumizi ya Ofisi Mtandao ( e-Office) kwa asilimia mia moja pamoja na operesheni nyingine”.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali akatoa rai na angalizo kuhusu matumizi ya Tehama au kufanya kazi kijiditali.
Pale aliposema .“Kuhusu matumizi ya tehama kama nilivyoeleza, jitihada za kupata vitendea kazi hivi ilikuwa walau kuiwezesha Ofisi kuweka mazingira bora kwa kila mtumishi kwamba, anafanya kazi zake kijiditali kwa hiyo Ofisi kwa sasa imetimiza wajibu wake wa kuwapatia watendaji vitenda kazi kwa zaidi ya asilimia 90”. Akasema
Na kuongeza “tulipokutana kwenye Baraza la Mwaka jana (2022) Mawakili wetu wa Mikoa hawakuwa na vishikwambi wala kumputa mpakato kwa sasa wote wanakumputa Mpakato”
Na katika kuhakikisha kwamba kila mtumishi anauwezo na maarifa ya kutumia vifaa hivyo vya TEHAMA, Mwenyekiti wa Baraza Dk.t Feleshi aliwaeleza wajumbe wa Baraza kwamba Ofisi imekamilisha tathimini ya ndani na akatumia nafasi hiyo kukipongeza Kitengo cha TEHAMA cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kukamilisha zoezi hilo la tathimini zoezi ambalo limebaini kwamba ni watumishi wanne tu ambao hawana maarifa ya kutosha ya kutumia vifaa vya TEHAMA.
Akasisitiza tena kwa kusema. “Kwa hiyo Wajumbe wa Baraza eneo hilo la matumizi ya TEHAMA na kutekeleza majukumu yetu kijiditali ni moja wapo ya eneo nililosema ikifika Julai Mosi 2023 litatosha kumuondoa Mtumishi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali”.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali akatumia fursa hiyo kuwashukuru wadau wote ambao wamesaidia na wanaendelea kuisaidia vitendea kazi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali huku akitoa shukrani za pekee kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.