MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA MBALIMBALI WA MWAKA 2024 WATUA BUNGENI

Imewekwa: 02 Sep, 2024
MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA MBALIMBALI WA MWAKA 2024 WATUA BUNGENI

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari amewasilisha mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2024 [ The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2024], Muswada huo umewasilishwa tarehe 2 Septemba 2024 Bungeni Jijini Dodoma.

Akisoma Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2024 [ The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2024], Mhe. Johari amesema Muswada huo unapendekeza kufanya Marekebisho katika Sheria za; Sheria ya Usimamizi wa Maendeleo ya Uvuvi wa Bahari Kuu, Sura ya 388 [The Deep-Sea Fisheries Management and Development Act, Cap 388], Sheria ya Madini sura ya 123 [ The Mining Act, Cap 123] na Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania, Sura ya 280 [The Tanzania Fisheries Research Institute Act, Cap 280]. 

Aidha Mwanasheria Mkuu ameeleza kuwa Muswada huo unapendekeza Marekebisho katika Sheria ya Usimamizi na Maendeleo ya Uvuvi katika Bahari Kuu Sura ya 388, ambapo amesema Sheria hiyo ilitungwa Mwaka 2020 baada ya kufutwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Bahari Kuu ya Mwaka 1998, Sheria hiyo haijawahi kufanyiwa marekebisho hivyo Merekebisho yanayopendekezwa katika sheria hiyo ni ya kwanza. 

“Mhe. Spika, Ibara ya Nne ya Muswada ikisomwa pamoja na aya ya B ya Jedwali la Marekebisho inapendekeza Marekebisho katika kifungu cha 11 kwa madhumuni ya kuainisha Mamlaka ya Uteuzi wa Wajumbe wa Kamati ya Wataalamu ya ushauri walioainishwa katika aya za C, D, E na F, na kubainisha muda wao wa kuhudumu kama Wajumbe wa kamati, hivyo inapendekezwa kwamba wajumbe tajwa wateuliwe na Waziri mwenye dhamana ya Uvuvi na kuhudumu kwa kipindi cha miaka mitatu”.

Vilevile vifungu vingine vilivyofanyiwa Merekebisho katika Sheria hiyo ni Kifungu cha 16 (1) ambacho kimependekeza kufutwa na kuandikwa upya kwa aya N ili kumpa Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya kuteua Maofisa wa utoaji leseni, Wakaguzi wa Uvuvi na Maafisa walioidhinishwa kutoka miongoni mwa Watumishi wa Mamlaka na kuteua Waangalizi wa Uvuvi waliopo katika Mamlaka au nje ya Mamlaka. 

Pia Marekebisho hayo yamegusa kifungu cha 35 cha Sheria hiyo ili kuleta masharti yanayoanzisha kosa la kujihusisha na shughuli zote za Uvivu wa Bahari Kuu bila kibali halali.

Muswada huo unapendekeza kufanya Marekebisho katika Sheria ya Madini, Sura ya 123 ambayo ilitungwa Mwaka 2010, Sheria hii imeshafanyiwa marekebisho mara 13, vifungu kumi na mbili (12) vimependekezwa kufanyiwa Marekebisho katika Sheria hii, huku ikiongezwa vifungu vipya viwili (2). Katika Sheria hiyo vifungu vilivyokusudiwa kufanyiwa Marekebisho ni Vifungu vya 4, 8, 27F, 66, 73, 86A, 87, 88,90A, 100C, 100D na 106, aidha vifungu vipya vinavyopendekezwa kuongeza ni kifungu cha 5B na 27I.

Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameelezea Marekebisho katika Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania, Sura ya 280, ambapo amesema Muswada unapendekeza Marekebisho katika kifungu cha 21 cha Sheria hiyo ili kuongeza maneno ya nyongeza mwishoni mwa kifungu hicho yanayoweka bayana usitishwaji wa kibali cha utafiti ikiwa kutakuwa na ukiwakwaji wa masharti ya utafiti. 

Muswada huo pia umependekeza kufutwa kwa kifungu cha 24 cha Sheria ya Utafiti wa Uvivu Tanzania Sura ya 280, kwakua Mamlaka aliyopewa Mkurugenzi wa Uvuvi yanakinzana na Mamlaka yaliyotolewa kwa Bodi.

Akimalizia katika kuwasilisha Muswada huo Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliwashukuru, Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kuandaa Muswada huo, aliipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria kwa kuuchambua Muswada huo kiweledi huku akiliomba Bunge kujadili na kupitisha Muswada ili kuyafanya Marekebisho hayo kuwa sehemu ya Sheria za nchi. 

“Mhe. Spika baada ya maelezo haya kwa mujibu wa Kanuni ya 99 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Mwaka 2023, ninaomba kutoa hoja kwamba Muswada huu wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2024 [ The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2024], kama ulivyo rekebishwa kupitia jedwali la Marekebisho ujadiliwe na kupitishwa katika hatua kusomwa kwa mara ya pili na ya tatu na hatimae marekebisho yanayopendekezwa yawe sehemu ya Sheria ya Nchi”.