MKANDARASI JENGO LA MWANZA ASHAURI KUANZA MCHAKATO WA LIFT

Na Mwandishi wetu
20 Septemba 2022
Mkandarasi (SUMA JKT)anayejenga jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo la Buswero Mkoani Mwanza , ameushauri uongozi wa OMMS kuanza mapema mchakato wa ununuzi wa lifti kwaajili ya matumizi jengo hilo.
Ushauri huo umetolewa jana ( jumatatu) na Luteni Kanali Mhandisi Fabian Buberwa kutoka SUMA JKT wakati alipokuwa akitoa maelezo kwa Mkurugenzi wa Mipango wa OMMS Bw Buji Bampabuye kuhusu maendeleo ya Ujenzi wa mradi
Mkurugenzi Bampabuye anakagua maendeleo ya mradi huo kwa maelekezo ya Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evaristo Longopa ili kupata taarifa za kina na za uhakika za maendeleo ya mradi huo.
Kwa mujibu wa M Mkandarasi Buberwa ambaye pia ni Meneja wa Kanda wa Suma JKT kwamba kwa uzoefu wake mchakato wa kununua lift hushukua kati ya miezi miwili hadi mitatu baada ya jengo kukamilika hivyo ni vema mchakato huo ukaanza mapema.
Kuhusu maendeleo ya mradi huo ambao hadi kukamililka kwake utagharimi Shilingi Bilioni 3. Lt Col Buberwa amesema kwa ujumla ujenzi wa jengo hilo lenye gorofa tatu unakwenza vizuri na matarajio ni likamilike kwa wakati au kabla ya wakati kulingana na mkataba.
“Matarajio yetu ni jengo litakamilike mapema sana mpaka ifikapo Mwezi Desemba mwaka huu ujenzi labda unaweza kukamilika na umaliziaji ( finishing) kati ya februari au Machi, lengo letu ni kukabidhi jengo mwezi March 2023. Nitoe ushauri kwamba mchakato wa manunuzi ya lift uanze mapema kwasababu mchakato wake kwa uzoefu wangu huweza kuchukua kati ya mienzi mitatu hadi mine”. Amesema Lt Col Buberwa.
Akielezea zaidi umuhimu kuanza mchakato huo mapema, Msimamizi wa Mradi huo Lt. Col Buberwa amesema jengo hilo halina njia ya watu wenye ulemavu kwa hiyo tegemeo kubwa na uwepo wa Lift.
Mkandarasi huyo amesema hadi sasa gorofa ya chini ( ground floor) imeshakamilika kwa kujenga matofali floor yote na vyumba vyote katika floor hiyo vimekamilika.
“Zege katika floor ya kwanza limeshamwaga na tarehe 20 septemba 2022 tutataanza kufanya setting ya gorofa ya pili ikiwamo kazi ya kusuka nondo na slabu ya gorofa ya pili, lakini niseme kwamba kazi ya ujenzi wa kuta za floor ya kwanza inakwenda sambamba na setting ya floor ya pili”. Akabinisha.
Amesema ujenzi wa mradi huo unakwenda kwa kasi kutokana na ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka kwa mwenye mradi( OMMS) na hasa suala la ufuatiliaji wa mara kwa mara
“Nawashukuru sana OMMS kwa kuja mara kwa mara kututembelea. Nimefanya kazi hii kwa miaka 15 lakini sijaona ushirikiano kama huu wa OMMS ni mradi wa kwanza ninaoufurahia kuusimamia na ndiyo mrdsi ambao naamini utakamilika mapema zaidi. Ninayo miradi hapa ina miaka mine haijakamilika, nyinyi mmeanza juzi tu lakini mradi unakwenda vizuri”. Amebainisha Lt. Col Buberwa
Amefafanua zaidi kwa kusema ushirikiano huu naupata pia kutoka kwa Mkuu wa Taasisi. “Namshukuru sana Mhe. Mwanasharia Mkuu wa Serikali amewahi pia kunipigia simu na kuuliza kama kuna changamoto yoyote katika mradi, hili halijawahi kutokea kwa kiongozi yoyote. Hii inatupa ari ya kuendelea kuchapa kazi na tunalipwa kwa wakati”
Kwa upande wake Mhandisi Mkazi wa Mkoa wa mwanza. Bw. Mosses Urio kutoka TBA yeye amesema kwa sasa hakuna changamoto yoyote na jengo anatarajia likamilike kwa wakati licha ya kuwa nyuma kwa siku 4 ambazo wameelekeza mkandarasi kuzifidia katika hatua ya ujenzi wa floor ya pili.
Akaongeza kwa kusema, wanahakikisha specimen zote zinapimwa chini ya usimamizi wao, kuwa na vikao vya mara kwa mara na kwa wakati na kwamba Mkandarasi anaendelea vizuri na hakuna deni lolote analodai.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi Bampebuye amepongeza kwa hatua nzuri ya ujenzi ya mradi huo na kuwahakikisha ushirikiano ili mradi ukamilike kwa wakati kama alivyoahidi.
Jengo la OMMS linalojengwa Mkoani Mwanza kwa usimamizi wa OMMS ni Jengo la Kwanza Jumuishi litakalotumiwa pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.