MHAGAMA AWATAKA SUMA-JKT KUKAMILISHA MIRADI YA SERIKALI KWA WAKATI

MHAGAMA AWATAKA SUMA-JKT KUKAMILISHA MIRADI YA SERIKALI KWA WAKATI
Na Mwandishi Maalum
DODOMA- Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama (Mb) ameitaka Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT kuhakikisha inatekeleza kwa wakati na kwa ukamilifu miradi ya ujenzi ambayo kampuni hiyo inapewa na Serikali.
Akasema ni kwa kufanya hivyo ndipo ambapo Kampuni hiyo itaendelea kuaminiwa na Serikali na kupewa miradi Zaidi ya ujenzi.
Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki ( Jumamosi) wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali . Jengo hilo linajengwa na Kampuni ya Ujenzi ya Suma JKT katika Mji wa Serikali Mtumba Mkoani Dodoma.
Akiwa katika Mtaa wa Mwanasheria , mtaa ambao ndipo linapojengwa jengo hilo na kupokelewa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evaristo Longopa, Waziri Jenista Mhagama alionyesha kutoridhishwa kwake na kasi ya utekelezaji wa mradi huo ambao kwa mujibu wa Mkandarasi na Mshauri Muelekezi mradi ya umefikia asilimia 55 ya ujenzi huku ukiwa upo nyuma kwa siku 60.
Baada ya kupokea taarifa hiyo fupi, Waziri Jenista Mhagama alisema. “Hapana naona kuna shinda, mkandarasi lazima ujitathimini na upitie upya ratiba ya utekelezaji wa mradi huu, mpango wa serikali nikuona mradi wa ujenzi wa Majengo ya Wizara na Taasisi unakamilika kabla ya kufika tarehe 9/12/2023. Kwa maelezo yako Mhandisi Muelekezi na Mkandarasi Napata shaka kama Jengo hili linaweza kukamilika kabla ya mwezi desemba mwaka huu” akasema Mhe. Mhagama
Na kuongeza “ Suma JKT, Serikali inawapatia miradi mingi ya ujenzi siyo tu huu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali bali pia katika maeneo tofauti tofauti nchini, na inaonekana kuna shida mahali miradi mingi haiendi kwa wakati, niwaombe sana mujifanyie tathimini na kupitia tena ratiba za miradi yenu ukiwemo huu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili Pamoja na mambo megine Serikali iendelee kuwaamini na kuwapatia miradi mingine.
Pamoja na kuwataka SUMA JKT kujitathmini Waziri Jenista Mhagama amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni Ofisi kubwa ambayo inapaswa mambo yake Kwenda sawa kama ilivyo Ofisi yenyewe.
Na kwasababu hiyo ameitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo huku akisisitiza kwamba jengo hilo linatakiwa kukamilika na kuanza kutumia kabla ya Mwezi Desemba 2023.
“Mhe. Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali niwaombe sana mfuatilie kwa karibu utekelezaji wa mradi huu, Ofisi hii ni kubwa, nitarudi tena kufuatilia na kuona kama maelekezo niliyotoa yamefanyiwa kazi. Mfuatilieni mkandarasi kazi ambazo zinaweza kufanyika kwa wakati mmoja bila shida ziendelee, niwaombe sana pia mzingatie sana thamani ya fedha katika utekezaji wa mradi huu na kubwa Zaidi nawatakia kila la kheri”. Akasema Waziri Mhagama.
Kwa upande wake Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evaristo Longopa akiwa ameambatana na watendaji wengine kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali alimshukuru Waziri Jenista Mhagama kwa kutenga muda wake na kuutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Makao Makuu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Na akatumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya awamu na Tano na Sita kwa uthumbutu wa kujenga mji wa serikali mradi ambao umechangia sana kubadilisha hadhi na taswira ya Mkoa wa Dodoma
Dkt. Longopa amemhakikishia Waziri kuwa kwa kasi inayoendelea hivi sasa ya umaliziaji wa baadhi ya kazi za ndani Pamoja na uwekezaji wa mifumo mbalimbali Jengo hilo linaweza kuanza kutumika kabla ya mwezi Desemba.
Aidha Meneja wa SUMA JKT Kanda ya Kati Meja Samule Jambo amemuhakikisha Mhe. Waziri kwamba jengo hilo litakamilika kabla ya mwezi Desemba 2023.
Mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hadi kukamilika kwake unatarajiwa kugharimu Tsh Bn 26.8. matarajio ya mradi ni kukamilika kabla ya septemba 2023.
Pamoja na kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali , Waziri Jenista Mhagama pia alitembelea na kukagua eneo la ujenzi Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Eneo la Ujenzi wa Uwanja wa Mashujaa, Wizara ya Maliasili na Utalii na Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge na Uratibu.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano
6/5/2023