MCHAKATO WA UREKEBU WA SHERIA KUU KUKAMILIKA MARCHI 2023.

MCHAKATO WA UREKEBU WA SHERIA KUU KUKAMILIKA MARCHI 2023.
Na Mwandishi Maalumu
Iringa
Mwandishi Mkuu wa Sheria Bw. Onorius Njole amewataka washiriki wa kikao kazi ambacho kimeanza mchakato wa mwisho wa kukamilisha zoezi la urekebu wa Sheria Kuu kuhakikisha wanaukamilisha mchakato huo kwa wakati na kwa viwango vya hali ya juu.
Ameyasema hayo leo jumamosi(March 4,2023) wakati akifungua rasmi shughuli za kikao kazi hicho kinachofanyika katika Hotel ya Mt.Royal Villa Mkoani Iringa, kikao ambacho washiriki wake ni kutoka Divisheni ya Uandishi wa Sheria Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Bw. Njore amewataka Mawakili hao wa Serikali ambao miongoni mwao ni waandishi wakuu wa sheria, waandishi washeria waadamizi, mawakili wa serikali na warekebu wa sheria kuhakikisha kuwa katika umoja wao siyo tu wanakuwa na uelewa wa pamoja wa ukamilishaji wa mchakato mzima wa urekebu wa sheria lakini wanatoa sheria zitakazokuwa na viwango na ubora wa hali ya juu.
“ Niwasihi sana ushiriki wenu katika mchakato huu mzima wa urekebu wa sheria si jambo dogo, ni ushiriki muhimu sana kwa mustakabali wa tasna ya sheria katika nchi yetu, lakini kupitia kwenu nchi yetu itapata sheria ambazo siyo tu zitakuwa katika juzuu moja bali pia zenye viwango vya hali ya juu viwango ambavyo vimetokana na umakini na uadilifu wenu”. Akasisiza Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Pamoja na kuwasisitiza washiriki wa Kikao kazi hicho kuhakikisha sheria zilizofanyiwa urekebo zinakuwa za viwango.
Amewasihi wataalamu hao kwamba zoezi la urekebu wa sheria zote kuu takribani 446 linatakiwa kukamilika mwezi huu wa Marchi 2023.
Katika kikao kazi cha wataalamu hao wa uandishi na urekebu wa sheria ambao wote ni kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiwamo Mawakili wa Serikali ambao wameajiriwa hivi karibuni wamepitia na kujadili kipengele kwa kipengele cha muongozo wa mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa mchakato mzima wa urekebu wa sheria na hasa katika uandishi wa sheria hizo.
Mapendekezo ya muongozo wa mambo muhimu ya kuzingatia katika mchakato mzima wa urekebu wa sheria uliwasilishwa na Mwandishi Mwandamizi wa Sheria Wakili wa Serikali Bwa. Shabani Kagunga.
Muongozo huo utawasaidia wataalamu hao kuwa na uelewa wa pamoja, uelewa ambao mwishoni utapelekea sheria zote ambazo zitakuwa zimefanyika urekebu kuwa na mwonekano unaofanana.
Pamoja na kupitia na kujadili muongozo huo, watakuwa na kazi kubwa ya kuzipita sheria zote ambazo zimefanyiwa urekebu kwa kuzingatia muongozo huo lakini pia watakuwa na jukumu la kuandaa nyaraka mbalimbali ukiwamo muswada unaohusiana na mchakato mzima wa zoezi hilo la urekebu wa sheria.
Mwandishi wa Habari hizi na ambaye amehudhuria kwa mara ya kwanza shughuli za urekebu wa sheria ameshuhudia namna ambavyo wataalamu hao walivyokuwa wakijadiliana na kupingana kwa hoja hadi kufikia muafaka wa nini walichoamini kinapaswa kuwa kifungu sahihi kuwepo ndani ya muongozo huo ili yawe sehemu ya muongozo wa kushughulikia masuala mbalimbali kabla ya kuandaliwa muswada wa marekebisho ya sheria zilizorekebiwa.
Kwa upande wake Mwandishi wa Sheria Mkuu mstaafu Bi. Grace Mfinanga anayeshiriki zoezi hili na kuchangia uzoefu wake, pamoja na mambo mengine, amewataka mawakili hao wa serikali wanaoshiriki jukumu hilo kuonyesha uadilifu na uaminifu wa hali ya juu wakati wote wa kutekeleza jukumu hilo.
Akasema uandishi wa sheria na urekebu wa sheria siyo jukumu la mchezo na kwamba linahitaji usiri wa hali ya juu sana na kuwataka kujisikia Fahari kuwa sehemu ya zoezi hilo.
Pamoja na kuzipitia tena sheria hizo kuu, kikosi kazi hicho pia kitakuwa na jukumu kama ilivyoelezwa wali la kuandaa nyaraka na matangazo mbalimbali yatakayotolewa sambamba na toleo la urekebu wa sheria pamoja na muswada wa marekebisho ya sheria ambazo zitahusika katika toleo la sheria zilizorekebiwa la mwaka 2023.
Zoezi la urekebu wa sheria kuu na ambalo limekuwa likitekelezwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Divisheni yake ya Uandishi wa Sheria na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali lilianza mwaka 2020 kwa hatua za awali na linagharimiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia mia moja.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano
4/3/2023