MAWAKILI WA SERIKALI WAPONGEZWA KWA KUTOA HUDUMA ZA KISHERIA BURE KWA WANANCHI

Imewekwa: 15 Apr, 2025
MAWAKILI WA SERIKALI WAPONGEZWA KWA KUTOA HUDUMA ZA KISHERIA BURE KWA WANANCHI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko amewapongeza Mawakili wa Serikali kwa kutoa huduma za kisheria bure kwa wananchi kupitia Kliniki za Kisheria katika mikoa mbalimbali nchini. 

Dkt. Biteko ameyasema hayo wakati alipokuwa Mgeni Rasmi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama Cha Mawakili wa Serikali tarehe 15 Aprili, 2025 Jijini Dodoma.
 
Akizungumza katika Mkutano huo Naibu Waziri Mkuu amefurahishwa na hatua za Mawakili wa Serikali za kutoa huduma za kisheria bila malipo kwa kuwa ni hatua sahihi katika kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi.

“Nichukue nafasi hii kuwapongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kufanya mikutano na kufanya kliniki za kutoa huduma za kisheria katika mikoa ya Dodoma, Kilimanjaro na Mwanza.” Amesema Naibu Waziri Mkuu.

Aidha, Mhe. Biteko amewakumbusha Mawakili wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na haki katika kutoa huduma kwa wananchi, huku akiwakumbusha kutoa ushauri sahihi pindi wanapoishauri Serikali kwenye masuala mbalimbali.

“Ifanyeni haki kuwa rafiki yenu na kila anayetoka mbele yenu atoke na tabasamu kuwa haki nimeiona ikitendeka.” Amesisitiza Mhe. Biteko.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari akizungumza katika Mkutano huo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa katika kukilea chama cha Mawakili wa Serikali kwa ufadhili anaoutoa.

“Nichukue fursa hii kumshukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kukilea chama chetu kwa kipindi cha miaka mitatu tangu amekizindua na sisi wajibu wetu kuhakikisha tunasonga mbele na hatutamuangusha.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Mhe. Johari amesema kuwa Mkutano huo ni fursa kwa wanachama kujadili masuala mbalimbali yanayohusu chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania, maendeleo ya sekta ya sheria kwa ujumla pamoja na kufanya uchaguzi wa viongozi wa chama cha mawakili wa Serikali.

Vilevile Mwanasheria Mkuu amewakumbusha Mawakili wa Serikali kuwa kauli mbiu ya mkutano huo inawataka Mawakili wa Serikali kuhakikisha wanasimamia vyema Utawala wa Sheria katika maeneo yao. Aidha, inawakumbusha watumishi na viongozi wa umma kuzingatia sheria wakati wanatekeleza majukumu yao kwani bila kuzingatia sheria, inaweza kuwa vigumu kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.

“Kauli mbiu yetu ya mwaka huu inatutaka Mawakili wa Serikali kuzingatia sana utawala wa sheria na kujipanga katika kutekeleza majukumju yetu kuelekea kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050”. Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini, akizungumza wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi amesema kuwa Wizara ya Katiba na Sheria itahakikisha kuwa inaendelea kushirikiana na Chama cha Mawakili wa Serikali na kuweka mazingira mazuri yatakayowezesha Mawakili hao kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa usahihi.

Naye, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Dkt. Talibu Mwinyi Haji akitoa salamu fupi katika Mkutano wa Chama cha Mawakili wa Serikali amemshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kumwalika kuja kushiriki katika mkutano huo, huku akiweka bayana kuwa mwaliko huo ni ishara ya mahusiano na mashirikiano mazuri yaliyoko baina ya Ofisi hizo mbili.

“Kipekee nimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutupatia mwaliko wa kushiriki mkutano huu mkubwa wa Mawakili wa Serikali, hii inaonyesha namna ambavyo Ofisi hizi mbili zinafanya kazi kwa kushirikiana kwa ukaribu mkubwa”. Amesema Dkt. Talib.

Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali umefanyika kwa siku mbili ambapo pamoja na mada mbalimbali zilizojadiliwa pia Mawakili wa Serikali wamepata fursa ya kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi mbalimbali wa chama hicho