MAWAKILI WA SERIKALI NA WAKUJITEGEMEA WAJENGEWA UWEZO KUHUSU MAHAKAMA YA AFRIKA MASHARIKI

WAJENGEWA UELEWA KUHUSU YA UTENDAJI KAZI WA EACJ
Na Mwandishi wetu
Mawakili wa Serikali sita (6) kutoka Taasisi za Kisheria za Serikali wamepata fursa ya kuhudhuria mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo na uelewa kuhusu majukumu ya Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ).
Mafunzo hayo yamefanyika hivi karibu katika Hoteli Serena Mkoani Dar es Salaam ambako pamoja na Mawakili hao wa Serikali pia yalihudhuriwa na Mawakili 15 wa Kujitegemea.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Mafunzo hayo Dkt. Dafina Ndumbaro kutoka Divisheni ya Uratibu na Ushauri wa Kisheria ( DCAS) Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, anasema katika siku hizo washiriki wa walipata nafasi ya kujifunza masuala mbalimbli yanayohusiana na mahakama hiyo.
Baadhi ya masuala hayo ni Mkao (Set up) ya Mahakama,Mamlaka (Jurisdiction) ya EACJ,Nani anaweza kusimamia kesi katika mahakama hiyo na Muda sahihi wa kufungua shauri,
Dkt. Ndumbaro anaeleza kuwa, washiriki hao pia walielimishwa kuhusu Mamlaka ya Mahakama za nchi Mwanachama katika mashauri yanayohusu Jumuiya ya Afrika Mashariki na Utaratibu wa Kukata rufaa.
Vile vile Mawakili Serikali pamoja na wenzao wa kujitegemea pia walijengewa uwezo kuhusu Kanuni zinazotumika Katika Mahakama za nchi Mwanachama wanapotaka kuwasilisha kesi kwa ajili ya maamuzi katika Mahakama ya Afrika Mashariki (kwa mujibu wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mahariki).
“Mafunzo haya ingawa yalikuwa ya siku mbili lakini yalikuwa na umuhimu wa pekee kwetu kama mawakili wa serikali , ni mafunzo ambayo yametupa fursa ya kujifunza mambo mapya yatakayotusaidia katika utendaji kazi wetu wa kila siku”. Amesema Dkt. Ndumbaro
Mawakili wa Serikali sita waliohudhuria Mafunzo hayo ni Beno Sanga (PSA), Felister Lelo (SSA) kutoka OAG, Hannelore M. Mnyanga (PSA), na Jackline Kinyasi(SA) kutoka NPS,Victoria Lugendo (SA) na Francis Oswald (SA) kutoka OSG
Aidha Mawakili hao wa Serikali na Mawakili wa kujitegemea wameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuratibu mafunzo hayo kwa kushirikiana na Mahakama ya Afrika Mashariki.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano
31/5/2022