MAJALIWA AISHAURI OMMS KUSHUKA KWA WANANCHI

MAJALIWA AISHAURI OMMS KUSHUKA KWA WANANCHI
Na Mwandishi Wetu
27/4/2023
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameishauri Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuweka mifumo ya kuwafikia wananchi waliowengi wanaohitaji Msaada wa Kisheria.
Ametoa ushauri huo leo ( Alhamisi) wakati alipotembelea Banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali muda mfupi kabla ya uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ( Mama Samia Legal Aid Campaig), uzinduzi uliofanyika katika Ukumbi wa Chimwaga- Chuo Kikuu cha Dodoma.
Akiwa katika Banda hilo la OMMS, Mkurugenzi Msaidizi Ushauri wa Kisheria Harroun Matagane Pamoja na mambo mengine alimuelezea Mhe. Waziri Mkuu namna ambavyo Ofisi imekuwa ikipokea maombi ya msaada wa wa ushauri wa kisheria.
” Mhe Waziri Mkuu pamoja na ushauri wa kisheria tunaoutoa kwa Wizara na Taasisi za Serikali na Wadau wengine, pia tunapokea maombi kutoka kwa wananchi wanaoomba ushauri au msaada wa kisheria katika maeneo mbalimbali , kwa mafano katika kipindi cha Julai, 2022 hadi March 2023 maombi ya ushauri wa kisheria 812 yalipokelewa na kufanyiwa kazi. Kati ya maombi hayo 812, 149 yalitoka kwa wananchi” . Akaeleza Mkurugenzi Msaidizi Harroun Matagane
Baada ya taarifa hiyo, ndipo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotaka kufahamu kwa kina kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inao mfumo unaofika mpaka katika halmashauri ambako amesema ndiko waliko wananchi wengi.
Akasema ingependeza au ingefaa endapo Ofisi itaangalia uwezekano wa kuwa na mfumo huo wakuwafikia wananchi waliowengi wenye shinda za kisheria badala ya kuishia katika ngani ya mikoa tu.
Pamoja na ushauri huo Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kuipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa utekelezaji mzuri wa Majukumu yake. “ Ninatambua utekelezaji mzuri wa majukumu yenu na katika hili ninawapongeza sana”.
Aidha Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro alitoa ufafanuzi wa kwanini OMMS haijafika mpaka ngazi ya Wilaya akisema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inashirikiana kwa karibu na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali .
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu kuzindua kampeni hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ( Mb) alisema utekelezaji wa kampeni hiyo unatokana na ridhio la Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania ambaye wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali uliofanyika Septemba 29,2022 Mkoani Dodoma aliridhia jina lake kutumika katika Kampeni hiyo.
Akizungumzia Zaidi kuhusu utekelezaji wa kampeni hiyo, Waziri Ndumbaro amesema Wizara itashirikiana na Wizara na Taasisi mbaliambli za Serikali na Wadau wengine wa ndani na nje.
Baadhi ya Taasisi za Serikali ambazo Mhe. Waziri alisema zitashiriki katika zoezi hilo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha baada ya uzinduzi uliofanyika leo huduma za ushauri na msaada wa kisheria zitaanza kutolewa katika Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma na Halmashauri zake viwamo baadhi ya vituo vya polisi na magereza zoezi litakalokwenda hadi tarehe 7/5/2023. Kwa mkoa wa Dodoma
Akasema baada ya mkoa wa Dodoma, Mikoa itakayofuatia ni Shinyanga, Manyara na Ruvuma na ratiba kwa mikoa mingine itatangazwa baadaye. Aidha kampeni hii itafanyika pia Visiwani Zanzibar na Pemba.
Akizindua Kampeni Mama Samia Legal Aid Campaign ni mpango wa miaka mitatu.
Kwa upande wake Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua Kampeni hiyo ametoa wito kwa wananchi wanaohitaji ushauri na msaada wa kisheria kuitumia fursa hii na hasa kwa kuwa ni bure na itawafikia wananchi pale walipo.
Akawataka viongozi wote katika ngazi mbalimbali wakiwamo wa Taasisi za Dini kutoa ushirikiano ikiwa ni Pamoja na kutoa taarifa zinazohusu matukio ya kikatili yanayofanyika katika maeneo yao husani wanawake, Watoto na makundi mengine yaliyokatika mazingira magumu.
Aidha amewataka na kuwahimiza viongozi hao kutoa taarifa za uwepo mambo yasiyozingatia maadili na utamaduni na mila za kitanzania katika maeneo yao na pia kutowafisha watuhumiwa.
Kauli mbiu ya Kampeni hii ni “Msaada Wa Kisheria Kwa Haki, Usawa Amani na Maendeleo”
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano