MAFUNZO YAWEZESHE WATAALAM KUISHAURI SERIKALI VIZURI-DKT. LONGOPA

MAFUNZO YAWEZESHE WATAALAM KUISHAURI SERIKALI VIZURI-DKT. LONGOPA
Na Mwandishi wetu
Dodoma
13 Septemba 2022
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evalisto Longopa amewataka maafisa wa serikali wanaoshiriki mafunzo ya kuwajengea uwezo katika maeneo ya gesi, madini na mafuta kuitumia vema fursa hiyo ili waweze kuishauri vema Serikali.
Ameyasema hayo leo jumanne wakati akifungua mafunzo ya siku nne yanayoratibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuendeshwa na Taasisi ya Kimataifa ya Afican Legal Support Facitility ambayo ipo chini ya Bank ya Maendeleo ya Afrika.
Mafunzo hayo yanafanyika katika ukumbi wa Igada uliopo katika Hoteli ya Dodoma, Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na mawakili wa serikali, wataalamu wa masuala ya jiolojia, wahandisi, wachumi na wataalamu wa masuala ya fedha ambapo katika siku ya kwanza watalaamu zaidi ya 30 wanashiriki.
Dkt. Longopa amesema, mafunzo hayo wamewezekana baada ya majadiliano ya muda mrefu na ya kina baina ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bank ya Maendeleo ya Afrika kuhusu ufadhili wa program za mafunzo ambazo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inakusudia kutekeleza.
Ni kufuatia majadiliano hayo AfDB iliweza kuipatia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mkopo nafuu wa kuendesha program hizo kupitia ALSF.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amebainisha zaidi kuwa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wataalamu kutoka taasisi za serikali yamegawanyika katika awamu tatu
Kwa mujibu wa Dkt. Longopa awamu kwanza na ambayo mafunzo yake yameanza ni kuhusu masuala ya madini, gesi na mafuta, awamu ya pili itahusu miradi ya ubia kati ya Serikali na makampuni binafsi (PPP)na na awamu ya tatu itahusu madeni ya Nchi.
“Ni matumaini yangu kwamba uwepo wenu leo na ushiriki wenu utawaongeza maarifa na kuwaweka katika nafasi nzuri ya kuishauri serikali, mhuwe huru kujadiliana na kubadilisha uzoefu ili kwa pamoja muweze kuisaidia Serikali katika kufikia maamuzi kwa manufaa ya maendeleo na nchi na watu wake” akasisitiza Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Awali Mratibu wa mafunzo hayo kutoka ALSF Bi. Manuela Dieng pamoja na kumshukuru Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa heshima ya kufungua mafunzo hayo amebainisha kwamba ALSF itaendelea kushirikiana na Tanzania kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo hilo la program za kuwajenge uwezo wataalamu katika maeneo mbalimbali.
Washiriki wa mafunzo haya pamoja na kufuatiliwa mada zinazowasilishwa pia wanapata nafasi ya kufanya majadiliano ya kina miongoni mwao kuhusu mada hizo pamoja na kuongezeana maarifa.