KLINIKI YA SHERIA BILA MALIPO YAZINDULIWA KILIMANJARO

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu amezindua rasmi Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro, tarehe 21 Januari, 2025 katika Ukumbi Mkubwa wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,
Uzinduzi huo, utafuatiwa na Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi inafanyika kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa wa Kilimanjaro. Huduma hizi zitatolewa katika Viwanja vya Stendi ya Vumbi jirani na Stendi Kuu ya Mabasi Moshi Mkoani Kilimanjaro kuanzia tarehe 21 hadi 27 Januari 2025.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Kliniki hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu ameipongeza na kuishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuuchagua Mkoa wa Kilimanjaro na kuja kutoa huduma ya Kliniki bure kwa wananchi wa Kilimanjaro.
"Tunaishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuja kutoa huduma hii bure kwa wananchi wetu hii inaonyesha namna Ofisi hii ilivyojikita kusogeza huduma kwa wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini". Amesema Mhe. Babu
Aidha, Mhe. Mkuu wa mkoa ameeleza kuwa Kliniki hiyo itasaidia kupunguza migogoro ya Wanachi dhidi ya Serikali, zitawezesha Mawakili wa Serikali kusimamia Utawala wa Sheria, pia zitawasaidia Mawakili wa Serikali kushirikiana kwa ukaribu na Wadau pamoja Wananchi katika kutatua masuala ya Kisheria.
"Leo tunakwenda kuanza Kliniki ya Sheria ni matumaini yangu itawasaidia wananchi wenye matatizo ya kisheria, kuna timu nzuri kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itakuwa inatatua changamoto mbalimbali za wananchi". Amesema Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ametoa wito kwa Wananchi wa Mkoa huo kushiriki kwa wingi katika Kliniki hiyo ili wapate suluhu ya changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili
Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi. Tamari Mndeme amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga vyema kutoa huduma za Kisheria bure kwa wananchi kupitia Kliniki hiyo.
"Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko tayari kuwahudumia Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na tuna wataalamu wa kutosha tunaamini kupitia Kliniki hii changamoto mbalimbali za wananchi zitatatuliwa". Amesema Bi. Tamari.
Kliniki ya Sheria bila malipo kwa Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro ni mwendelezo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kusogeza huduma za Kisheria kwa Wananchi.