HUDUMA ZA KISHERIA KUWAFIKIA WANANCHI WALIPO-WAZIRI NDUMBARO

Na Mwandishi Maalum
Wizara ya Katiba na Sheria imeahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi zake katika kuhakikisha huduma za kisheria zinawafikia wananchi kwa wakati na mahali walipo.
Ahadi hiyo imetolewa hivi karibuni na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndubaro (Mb) wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la Jengo la Kituo Jumuishi la Taasisi za Kisheria za Serikali linalojengwa Mkoani Mwanza.
Waziri Ndumbaro ambaye alikuwa mgeni rasmi katika halfa hiyo amebainisha kuwa, Dira na Dhima za Wizara hiyo zinalenga kufanya upatikanaji wa haki nchini unakuwa mwepesi na wa haraka
Akinukuu Dira na Dhima ya Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Ndumbaro alisema.“ Dira inasema “ Katiba na Sheria Wezeshi kwa Maendeleo ya Taifa” na Dhima inayosema “Kuwa na Mfumo Madhubuti wa Kikatiba na Kisheria wenye kufanikisha mpango wa Maendeleo ya Taifa. Ni Dhahiri kuwa Dira na Dhima za Wizara zinalenga kufanya lengo la upatikanaji wa haki katika nchini yetu kuwa mwepesi na wa haraka”Akaeleza Waziri
Ni kwa sababu hiyo, akasema , Wizara imeendelea kuimarisha miuondombinu katika kuhakikisha upatikanaji wa haki unakua mwepesi na haraka kwa kila mwananchi.
“Kutokana na hili, nipende kutoa Shukrani kwa Serikali wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imeendelea kutoa fedha kwa Mahakama Pamoja na Taasisi nyingine za kisheria ambapo miradi mbalimbali imeendelea kujengwa ikiwemo ujenzi wa Vituo Jumuishi katika Mikoa mbali mbali”.
Pamoja na kuishukuru Serikali Kuu kwa kuendelea kutoa fedha kwaajili ya ujenzi wa vituo Jumuishi vya Taasisi za Kisheria za Serikali. Waziri Ndumbaro pia amempongeza na kumshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kufanikisha kuanza kwa ujenzi wa vituo jumuisha
“Nitumie fursa hii kukupongeza Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa jitihada na hatua ulizozichukua za kuhamasisha uwepo wa vituo jumuishi kwa lengo la kutoa huduma za kisheria katika eneo moja (one stop Centre). Si kila mtu anawezaa kuwa na wazo na kulitekeleza Hongera sana!.
Awali akimkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria kuweka jiwe la Msingi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali , Mhe. Jaji Dkt. Elizer Feleshi alieleza kuwa, hatua hiyo ya kuwa na Vituo Jumuishi kwaajili ya Taasisi za Serikali zinazotoa huduma za kisheria itapunguza gharama za uendeshaji.
“Kwa taasisi zote za kisheria kuwa katika Jengo moja, pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji, pia kutapunguza gharama kwa wadau wetu kwani wataweza kupata huduma katika jengo moja tofauti na ilivyo sasa”. Akasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akaongeza kuwa kwa kutambua changamoto inayozikabili Taasisi za kisheria ikiwamo ya kutokuwa na miundombinu ya Ofisi, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia wazo la kuwa na Mpango wa kujengwa kwa majengo yatakayokuwa Vituo Jumuishi vitakavyotumiwa na Taasisi za Kiserikali zinazotoa huduma za Kisheria.
“Hivyo uwekaji wa Jiwe la Msingi katika Kituo Jumuishi Mkoani Mwanza, ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe Rais Pamoja na maazimio ya Timu ya Serikali ya Sheria ambacho ndicho chombo pekee cha Kisheria kinachojadili masuala ya kimkakati na kufanya maazimio ya kuziwezesha Taasisi husika kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake” akasisitiza Mwanasheria Mkuu.
Akizungumzia matumizi ya Rasilimali zilizotumika katika ujenzi wa kituo hichyo, Mwanasheria Mkuu amebainisha kuwa matumizi yamehusisha fedha kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (fungu16) na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka fungu 35).
“ Ujenzi wa Majengo ya Vituo Jumuishi yanayojengwa katika mwaka huu wa fedha kupitia fungu 16 yakihusisha jengo hili la Ilemela Mwanza pamoja na Arusha ambapo kiwanja hiki cha Ilemela kinamilikiwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ( Fungu 35) huku fedha za ujenzi kwa ridhaa ya Mlipaji Mkuu wa Serikali zikitoka Fungu 16 yaani Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali”.
Jengo hilo ambalo ni la ghorofa tatu litakapokamilika litatumiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikalia na Ofisi ya Kabadhi Wasii Mkuu ( RITA)
Hafla ya uwekaji wa jiwe la Msingi ilihudhuriwa pia na Mhe. Dkt. Ntemi Nihimilwa Kilekamajenga, Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Dkt. Evaristo Longopa, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Khatibu Kazungu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Sylvesta Mwakitalu Mkurugenzi Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Dkt. Boniface Luhende Wakili Mkuu wa Serikali na Kabidhi Wasii Mkuu na Mtendaji Mkuu Bi. Anjela Anatory.