HESHIMA YA MAWAKILI WA SERIKALI HAIWEZI KUSHUKA KAMA MANA- WAZIRI NDUMBALO

Na Mwandishi Maalum
3/11/2022
DODOMA
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbalo (Mb) amesema, heshima na hadhi ya mawakili wa serikali haiwezi kushuka kama mana bali ni kwa uongozi wa Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA)) kuhakikisha heshima hiyo na hadhi vinarejea kwa Mawakili wa Serikali nchini.
Ameyasema hayo leo ( Alhamisi) wakati ujumbe wa viongozi wa Chama hicho ukiongozwa na Rais wa Chama hicho Wakili Msomi Michael Marcellus Luena ulipokwenda Ofisini kwake Mtumba, Jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha.
Chama cha Mawakili wa Serikali kilizinduliwa rasmi na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikai uliofanyika Septemba 29 Jijini Dodoma
Baada ya Mhe. Rais kuzindua Chama hicho. Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi kwa mamlaka aliyonayo aliteua viongozi wa mpito.
Viongozi walioteuliwa ni Wakili Msomi Michael Marcellus Luena ambaye ni Rais, Makamu Rais ni Wakili Msomi Lucas Charles Malunde, Mwenyekiti ni Wakili Msomi Stephano Seba Mbutu, Makamu mwenyekiti Wakili Msomi Hassan Mayunga, Katibu akiwa ni Wakili Msomi Sia Beatrice Mrema na mweka hazina Wakili Msomi Irene Joseph Luselie.
“Wanachama wenu wanataka kuona wanathaminiwa na wana hadhi , na hili haliwezi kushuka kama mana, ni moja ya kujukumu lenu kama viongozi pamoja na mambo mengine, kuwafanya wajisikie hivyo”. akasema Waziri Ndumbalo
Katika mazungumzo hayo na ambayo pia yalihudhuriwa na Katibu Mkuu Mary Makondo, Waziri Ndumbalo amebainisha kuwa katika nchi nyingine, Wakili wa Serikali au Mwanasheria wa Serikali anaheshima sana na anahadhi ya juu.
“ Kwa hiyo, mnakazi kubwa ya kufanya branding cha chama chenu lakini pia ya mawakili wa Serikali, Chama lazima kionekane kipo na kinafanya kazi.”akasisitiza Waziri.
Akielezea zaidi kuhusu kusafisha taswira ya Mawakili wa Serikali, Waziri wa Katiba na Sheria alitolea mfano kwa kusema
“ Jana ( jumatano) kulikuwa na mjadala mkali Bungeni kuhusu mikataba, mpaka ikaonekana wanasheria ni wa ovyo, lakini wakati mwingine shida si wanasheria kwa hiyo mnayo kazi ya kusafisha taswira ya wanasheria wa Serikali”
Ameutaka uongozi huo kuhakikisha , Mawakili wa Serikali popote walipo kutoruhusu mkataba wowote kutumia bila ya kupita kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali lakini pia kuhakikisha wanashirikishwa na kuhusika katika hatua zote zikiwamo za majadiliano ya mkataba huo.
Waziri Ndumbalo pia ameuagiza uongozi huo kutetea maslahi na stahiki za wanachama wao.
“Unakuta wakili wa serikali anasimama mahakamani kuitetea serikali kwenye kesi zinazohusu mabilioni ya fedha lakini hali yake kwa maana stahili zake na maslahi yake ni suala jingine hivyo mnaowajibu pia wa kulifanyia kazi hili la maslahi bora ya wanachama wenu.
Katika hatua nyingine Waziri Ndumbalo ameutaka uongozi huo kuwa na mahusiano ya karibu na Chama cha Mawakili Tanganyika ( TLS).
Vile vile amewataka viongozi hao kujenga mazingira mazuri yatakayokiwezesha Chama cha Mawakili wa Serikali kushiriki na kutoa mchango wao katika mijadala mbalimbali inayohusu masuala ya Sheria zikiwamo sheria zinazopelekwa Bungeni.
Awali Rais wa PBA Wakili Msomi Michael Luena akielezea nia ya ziara hiyo, alisema pamoja na kujitambulisha lakini pia wajumbe wameanza vikao vyao vya awali vya ambapo wanajadili masuala mbalimbali yanayohusu Chama hicho.
Viongozi hao pia wameahidi kuyafanyia masuala yaliyoainishwa na Waziri Ndumbalo kwa mstakabali wa chama na wanachma.
Mwisho.