BAJETI YA KUTOSHA ITATUWEZESHA KUTEKELEZA MAJUKUMU KWA WAKATI-AG FELESHI

BAJETI YA KUTOSHA ITATUWEZESHA KUTEKELEZA MAJUKUMU KWA WAKATI-AG FELESHI
Na Mwandishi wetu
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt Eliezer Feleshi ameelezea haja na umuhimu wa Ofisi kuwa na bajeti ya kutosha itakayoiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa tija, weledi na kwa wakati.
Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipoitembelea timu ya wataalamu inayopitia miongozo iliyoandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Timu hiyo na ambayo ipo chini ya Jaji Mstaafu Juxon Mlay inaendelea na jukumu hilo katika ukumbi wa Mikutano wa Mahakama ya Kisutu Mkoani Dar es Salaam
Mwanasheria Mkuu amewaeleza wataalamu hao kwamba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikiwa na bajeti ya kutosha itakuwa huru na itakuwa na uwezo mkubwa wa kuboresha maeneo mengi likiwamo eneo la kufanya tafiti zinazohusu masuala ya sheria, makubaliano ya kimataifa na kufanyia kazi maeneo mengine bila kusubiri maelekezo kutoka Serikalini.
“Tukiwa na bajeti ya kutosha itakuwa rahisi kwetu kufanya mambo mengi na kwa wakati, kwa mfano, tunaweza kufanya tafiti zinazohusu masuala ya sheria na hata kwa kazi za kuandika sheria na kutafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili tutaweza kuzifanya kwa wakati”. Akasema
Na kuongeza“ Matumini na hamu yangu kubwa ni kwa Ofisi hii kuwa na bajeti inayojitosheleza”
Pamoja na kuelezea hamu kubwa ya kutaka Ofisi iwe na Bajeti ya kutosha, Mwanasheria Mkuu Feleshi pia ameelezea kuridhishwa kwake na kazi inayofanywa na wataalamu hao ya kupitia miongozo hiyo.
“ Nitoe shukrani zangu za dhati kwenu, kwanza, kwa kukubali kwenu kuja kupitia na kutoa mawazo yenu ya kitaalamu kwenye miongozo hii ambayo . Nimeridhishwa na kufurahishwa na maendeleo ya kazi hii na ni matumaini yangu itakamilika kwa wakati
Akasisitiza kuwa maoni yaliyotolewa na wataalamu hao kuhusu miongozo hiyo ameyapokea na yataendelea kufanyiwa kazi.
Kwa upande wao wakiongea kwa nyakati tofauti, Watalaamu hao wameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuaandaa miongozo hiyo na kwa wao kupewa heshima ya kuifanyia kazi na kutoa mawazo yao.
Akitoa maoni yake, Jaji Mstaafu Juxon Mlay alikuwa na haya ya kusema “ Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali , sisi tunashukuru kwa kutukumbuka na kuona kwamba tunafaa kuipitia miongozo hii na kutoa maoni yetu ya kitaalamu”.
Akaeleza zaidi kwa kusema. “Tunashukuru pia kwa kuipitia miongozi hii tumepata fursa yakujikumbusha kwani nasi tuliwahi kufanya kazi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika nafasi mbalimbali, tumekutana tena na kukaa pamoja kuifanya kazi hii na kutoa mawazo yetu ni fursa na tunajisikia kuthaminiwa”.
Baadhi ya mapendekezo ya jumla waliyowasilisha ni pamoja na kutaka miongozo itoe maelekezo ya hatua kwa hatua yatakayomsaidia Wakili wa Serikali popote alipo kutekeleza majukumu yake kwa weledi na maarifa.
Aidha wameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuandaa miongozo hiyo ikiwa ni pamoja na kuanzisha Chama cha Mawakili wa Serikali.
Pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuitembelea timu hiyo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evaristo Longopa na Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole nao walipata nafasi ya kuitembelea timu hiyo na kuzungumza nao.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Feleshi aliunda timu ya wataalamu inayohusisha mawakili wa serikali waandamizi kwaajili ya kuipitia na kuiboresha miongozo ambayo imeandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla miongozo hiyo haijaanza kutumika.
Wataalamu hao ni Jaji Mstaafu Juxon Mlay ambaye amewahi kuwa Naibu Mwandishi Mkuu wa Sheria na Mkurugenzi wa Mashtaka, Jaji mstaafu Julius Malaba aliyewahi pia kuwa Mkurugenzi wa Divisheni ya Mikataba , Jaji mstaafu S. Bentram Matupa ambaye amewahi kuwa Katibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bi. Sarah Barahomoka aliyewahi kuwa Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Pia wapo Mawakili wa Serikali waandamizi kutoka Divisheni ya Uandishi wa Sheria, Divisheni ya Mikataba na Divisheni ya Uratibu na Ushauri wa Kisheria.