AG FELESHI ATOA WITO KWA TAASISI ZA KISHERIA ZA SERIKALI KUJIFANYIA TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YAO

DODOMA-Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Elizer Mbuki Feleshi amezitaka Taasisi za Kisheriaza Serikali kujifanyia tathimini ya utekelezaji wa majukumu yao na kutoa mapendekezo ya changamoto wanazokabiliana nazo ili zifanyiwe kazi.
Ametoa agizo hilo siku ya Jumatatu ( June 5/2023 )wakati akitoa salamu za pongezi kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kufikisha miaka mitano tangu kuundwa kwake mwaka 2018. Na mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.
Maadhimisho hayo yanakwenda sambamba na mafunzo ya kuwajengea uwezo na uelewa Mawakili wa Serikali kuhusu masuala mbalimbali yakiwamo ya uendeshaji wa kesi za madai, majadiliano na usuluhishi.
Mhe Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na kuzitaka Taasisi za Kisheria za Serikali kuiga mfano huo wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wa kujitathmini amewataka pia Mawakili wa Serikali nao kujifanyia tathmini.
Amekasema “ Ogopa sana tu ambaye kila kukicha ni kama jana, hakuna mabadiliko wakati nyakati zinabadilika hata magonjwa yanabadilika”.
Akasema yeye kama kiongozi Mkuu wa Mawakili wa Serikali takribani 3,449 moja ya jukumu lake la msingi ni kuhakikisha mawakili hao wa serikali wanakuwa wenye weledi, ubora na uwezo wa kutekeleza majukumu mtambuka.
Akisisitiza kuhusu nafasi yake ya Uongozi kwa Mawakili wote wa Serikali amezikumbusha Taasisi za Kisheria za Serikali na Mawakili wote wa Serikali kukumbuka kuwa wanatekelekeza majukumu yao kwa niaba yake.
“ Mhe. Mgeni Rasmi, Mimi ndiye kiongozi wa Mawakili wote wa Serikali ambao hadi June 3 tulikuwa 3450 lakini kwa sasa tupo 3449 baada ya Wakili Mmoja kufariki June 3 2023, sasa wakati nikiwapongeza Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kuadhimisha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake ikiwa ni pamoja na kujitafanyia tathmini, walipotoka walipo na wanapokwenda, nipende kuwakumbusha kwamba utekelezaji wa majukumu yao lazima utokane na uzingatie maelekezo yangu” akasisitiza na kuongeza.
“Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali nafikiri kuna jambo linalofanyika na vilevile Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. Hamuwezi kufanya jambo lolote nisifahamu na taasisi nyingine, kwa sababu kwa mujibu wa sharia hawa wote wanaleta taarifa zao kwangu na kupokea maelekezo kutoka kwangu”
Akasema angependa kutumia muda huo wa kutoa salamu zake kumwomba Wakili Mkuu wa Serikali kuwa hatekelezi majukumu yake bila kupata maelekezo kutoka kwa mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Ni muhimu sana Wakili Mkuu wa Serikali uwafundishe hasa Mawakili wapya wasije wakatekeleza majukumu yao bila maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali “. Akasisitiza Mhe. Feleshi.
Akizungumzia zaidi kuhusu miaka mitano ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Mhe. Feleshi amebainisha kwamba kama kuna mtu mwenye furaha basi ni yeye.
Akasema furaha yake hiyo inatokana na kushuhudia maboresho makubwa ambayo yamefanyika katika Tasnia ya Sheria hususani Taasisi za kisheria za Serikali maboresho ambayo amesema yameongeza tija na ufanisi mkubwa katika utoaji wa haki lakini pia katika kuisaidia serikali katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo na ustawi wao.
“ kama ni jeshini basi mimi ningekuwa Jenerali kutokana na kushuhudia mengi na kushiriki katika maboresho na mageuzi katika tasnia ya sharia hapa nchini. Nimeshuhudia na ninaushuhuda mkubwa wa tulikotoka tulipo na tunapoelekea basi niwaombe wenzagu tuyautumie maadhimisho haya pamoja na mafunzo kujijengea msingi bora na imara ya utekelezaji wa majukumu yetu” akasisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akawakumbusha Mawakili wa Serikali kauli ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyowaita Mawakili hao Septemba mwaka jana kuwa na Jeshi la kulinda uchumi wa Nchi kwa kutumia kalamu zao na taaluma yao.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano
5/6/2022