AG FELESHI AKUTANA NA WATAALAMU WA BSAAT

Na Mwandishi Wetu
Dodoma
8/12/2022
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi leo (Alhamisi) amekutana na kufanya mazungumzo na timu ya wataalamu inayofanya tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa Mapambano Endelevu dhidi ya Rushwa Tanzania (BSAAT).
Mazungumzo kati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na timu hiyo inayoundwa na Wataalamu kutoka Nchini Uingereza wakishirikiana na FCDO Pamoja na waratibu wa mradi huo kutoka Ofisi ya Rais Ikulu yamefanyika katika Ukumbi wa Mkutano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.
Akitambulisha wataalamu hao, Mratibu wa BSAAT Dkt. Bonaventura Baya alimueleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwamba, wataalamu hao wapo katika ziara ya kutathimini utekelezaji wa mradi wa mapambano endelevu dhidi ya Rushwa Tanzania ili kubaini mafanikio na changamoto.
Akabinisha kuwa imekuwa heshma kubwa kwa timu hiyo kupata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na wataalamu wake.
Katika mazungumzo hayo na ambayo yalichukua zaidi ya saa moja, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Feleshi pamoja na kuwasilisha tathmini yake na ushiriki wa Ofisi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika mradi huo, pia ameishukuru Timu hiyo ya Wataalamu kwa kumtembelea Ofisini kwake lakini pia kupata fursa ya kukaa ana kwa ana na wataalamu hao na kubalishana mawazo kuhusu mafaniko na changamoto katika utekelezaji wa Mradi huo.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilianza utekelezaji wa programu mbalimbali za BSAAT mwezi April mwaka huu kwa kuwa na vikao kazi vilivyofanyika katika Mikoa ya Mwanza, Iringa na Arusha.
Aidha baada ya vikao kazi hiyvo shughuli mbalimbali zimekuwa zikiendelea chini ya ufadhili wa BSAAT.
Katika mazungumzo hayo Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliambatana na Bi. Ndeonika Mwaikambo ambaye ni Mratibu wa Mradi huo katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Upendo Ndosi ( Mchumi) Bw. Meja Kulaya ( Mhasibu) na Bw. Fredy Nyaroga na Christopher Bwire ( IT)
Mradi wa Mapambano Endelevu dhidi ya Rushwa Tanzania ( BSAAT) unaratibiwa na Ofisi ya Rais Ikulu kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza na Jumuiya ya Ulaya