OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAKUTANA NA TLS MWANZA

Imewekwa: 14 Jun, 2025
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAKUTANA NA TLS MWANZA

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mwanza tarehe 13 Juni,2025 imekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Mwanza,  Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu mkoani Mwanza.

Akizungumza kuhusu kikao hicho Wakili wa Serikali mkoa wa Mwanza na Mwenyekiti wa kikao, Bw. Kabyemela S. Lushagara amesema kuwa Taasisi hicho zimekutana kwa lengo la kuifahamisha TLS mkoa wa Mwanza kuhusu uwepo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mkoa wa Mwanza  na huduma mbalimbali zinazotolewa na Ofisi hiyo.

Aidha, Bw. Lushagara amesema pia kikao hicho kimejadili namna ya kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizi mbili hasa katika kuwezesha Wananchi wasio na uwezo kupata msaada wa kisheria na uwakilishi Mahakamani. 

" Tumekutana hapa kwa lengo la kuendelea kujenga mahusiano na kupanga mikakati ya kutoa huduma bora kwa wananchi." Amesema Bw. Lushagara 

Katika hatua nyingine, Bw. Lushagara amesema kuwa kikao hicho kitaiwezesha Kamati ya Ushauri wa kisheria ya Mkoa wa Mwanza kuwapeleka kwa TLS Wananchi wanaohitaji msaada wa uwakilishi  Mahakamani  pale inapotokea wananchi hao wamepekeka malalamiko au maombi yao kwa Kamati. 

Kikao hicho kilihudhuriwa na Wakali, Joseph Mugabe(Chapter Converner), Wakili. Erick Mutta ( Vice- Chapter Converner) na Wakili Amri Linus( Chapter Coordinator).