OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI NA LAW SCHOOL KUSHIRIKIANA KATIKA MAFUNZO KWA VITENDO

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imesaini hati ya makubuliano na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) yenye lengo la kuwezesha Taasisi hizo kushirikiana katika masuala mbalimbali yanayohusu taaluma ya Sheria.
Hayo ameyasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza S. Johari tarehe 2 Julai, 2025 Jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya utiaji wa saini makubaliano baina ya Taasisi hizo, ambapo ameeleza kuwa makubaliano hayo yatasaidia kuwajengea uwezo wa kitaalamu wanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) katika masuala mbalimbali ya kisheria.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa makubaliano hayo yatawawezesha wanafunzi na wahitimu kutoka LST kushiriki katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria, kuongeza ujuzi, weledi, Ukuaji wa Kitaaluma na kuwajengea uwezo wa namna ya kuwasiliana na wateja pamoja na mahusiano baina ya Wakili na Mteja.
"Ushirikiano huu utasaidia katika kuboresha eneo la huduma ya msaada wa kisheria (LEGAL AID) eneo hili bado ni changamoto katika nchi yetu na sisi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Seriklj tumeona ni vyema tukaliimarisha ili wananchi waweze kupata huduma kupia vituo vya huduma contact centers ambazo tunazianzisha”. Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema pamoja na masuala mengine watakayoshirikiana ni kuwezesha taasisi hizo kushirikiana katika taaluma ya mafunzo, kutengeneza mafunzo wezeshi kwa wanafunzi na wahitimu wa taaluma hiyo pamoja na kushiriki kwenye huduma za msaada wa kisheria.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST), Prof. Sist Mramba, ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua hiyo kubwa itakayowawezesha wanafunzi wa chuo hicho kupata uzoefu na kuwafanya kuwa mahiri katika maeneo mbalimbali.
“Hii itakuwa fursa nzuri kwa wanafunzi wetu watakapokuwa wanashiriki kwenye zoezi la huduma ya msaada wa kisheria kwa watanzania watakuwa wanaendelea kunoa umahiri wao na kuleta uendelevu katika kutoa msaada wa kisheria.” Amesema Prof. Mramba
Hati ya Makubaliano baina ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Chuo cha Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) imesainiwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno na Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) Prof. Sist Mramba.