OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI MWANZA YAKUTANA NA MKANDARASI ANAYESIMAMIA UJENZI WA SGR LOT 5 (Mwanza - Isaka)

Wakili wa Serikali wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mwanza Bw. Kabyemela S. Lushagara amekutana na kufanya mazungumzo na Injinia Moga Kulwa Meneja Mradi Msaidizi anayehusika na Mradi wa ujenzi wa SGR LOT 5 (Mwanza - Isaka), tarehe 12 Juni, 2025 Ofisi kwake Jijini Mwanza.
Akizungumza kuhusu kikao hicho Bw. Lushagara amesema kuwa mazungumzo hayo yamelenga kupata taarifa za maendeleo ya mradi huo.
"Kikao chetu kililenga kupeana updates ya hatua zilizofikiwa katika ujenzi, kujadili changamoto zilizojitokeza na kushauriana namna ya kuondokana na changamoto hizo".
Aidha, Bw. Lushagara ameeleza kuwa kikao hicho ni mojawapo ya hatua za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kusimamia utekelezaji wa masharti ya Mikataba inayoingiwa na taasisi za Serikali katika Mkoa wa Mwanza ikiwa ni pamoja na Mikataba ya miradi ya Kimkakati, Uwekezaji na ya Maendeleo.
Vilevile, Bw. Lushagara amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mkoa wa Mwanza imeweka utaratibu wa kukutana mara kwa mara na Taasisi za Serikali zinazosimamia miradi mbalimbali Mkoni Mwanza kwa lengo la kushauriana na kufuatilia utekelezaji wa masharti ya Mikataba husika.
Mara baada ya kikao hicho Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mkoa wa Mwanza inakusudia kutembelea eneo la mradi kwa ajili ya kujionea mwenendo wa utekelezaji wa masharti ya Mkataba pamoja kushauriana juu ya namna bora ya kuzitatua changamoto za utekelezaji pindi zinakapojitokeza