OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA OFISI YA WAZIRI MKUU

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeahidi kuendeleza ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuimarisha utendaji kazi na kuboresha huduma kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Divisheni ya Uratibu na Ushauri wa Kisheria Bi. Neema Ringo akizungumza kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari tarehe 4 Julai, 2025 mara baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofanyika katika viwanja vya Julius Nyerere Sabasaba Jijini Dar es Salaam.
"Kipekee niipongeze Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaliko huu na sisi tunaahidi kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na ushirikiano wa hali ya juu katika kutoa huduma kwa wananchi. Amesema Bi. Ringo .
Akiwa katika banda hilo Mkurugenzi wa Divisheni ya Uratibu na Ushauri wa Kisheria amepata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ikiwa ni pamoja na miradi ya maendeleo, mipango ya kiutendaji ya Serikali, pamoja na mafanikio ya utekelezaji wa Sera na Programu mbalimbali chini ya ofisi hiyo.
Aidha, Bi. Ringo amezipongeza Taasisi mbalimbali zilizoko katika banda hilo kwa juhudi za kuhakikisha wananchi wanaotembelea katika Taasisi hizo wanapata elimu ya kutosha kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Serikali, hususan katika sekta za ajira, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, na uratibu wa shughuli za maafa.
"Niwapongeze kwa kuendelea kutoa elimu pia yatumieni maonesho haya kama jukwaa la Serikali kuwasiliana moja kwa moja na wananchi na kuwapa fursa ya kufahamu masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali". Amesema Bi. Ringo
Maonesho ya Sabasaba yalianza tarehe 28 Juni, 2025 yanaendelea hadi tarehe 13 Julai, 2025 na yamejumuisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, yakilenga kukuza biashara, ubunifu, na mahusiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma